The House of Favourite Newspapers

Si Mliamua Wenyewe Kuoana? Basi Vumilianeni!

0

NIANZE kwa kumshukuru Mungu kwa pumzi ambayo ameniwezesha kuendelea kuitumia bila malipo yoyote. Pole msomaji wangu wa XXLove ambaye unasumbuliwa na matatizo mbalimbali. Usikate tamaa, endelea kumuomba Mungu na kuamini kuwa atakusimamia.

Yapo mapito ya kila aina kwenye maisha ya ndoa. Kuna milima, mito, mabonde na tambarare. Kuna kipupwe na jua kali. Kuna masika na kiangazi, yote ni majira ambayo mwanadamu anapaswa kuyapitia katika maisha yake ya kila siku.

Kuna maisha ya furaha, karaha, amani, majuto, ugonjwa, chembechembe za usaliti au usaliti wenyewe, kukosa fedha, kufukuzwa kwenye nyumba mliyopanga na kuachishwa au kufukuzwa kazi kwa mkeo au mumeo. Hizi ni nyakati ambazo wanandoa mnapaswa kuzifahamu, kuzipitia na kuziishi.

Bila shaka somo hili litakufaa wewe uliye ndani ya ndoa na hata kama hujaingia kwa kuwa kuna siku utaingia, basi ni vyema ukasoma, ukaelewa na ukayaishi maneno haya kwa ajili ya kudumisha na kufikia malengo yako uliyokubaliana au utakayokubaliana na mwenza wako wakati mkifunga ndoa.

Kama kweli uliamua kuoa au kuolewa na mtu ambaye uliamini mnapendana, basi ni lazima mjifunze kuvumiliana majira na nyakati zote ngumu na rahisi ambazo mnakutana na mtakutana nazo katika maisha ya ndoa yenu.

Usiishi au usinung’unike kwa familia ya rafiki au jirani yako kuishi vizuri na kuona kama wewe pekee ndoa yako ndiyo ina matatizo, la hasha! Hata hao ambao unadhani wanaishi kwa furaha na upendo kila siku, kuna wakati wanakwazana, wanapishana, lakini kwa kuwa wanajua kuwa wao ni mke na mume, basi wao wanamaliza tofauti zao wenyewe na maisha yanasonga.

Unaweza ukaona kuwa familia ya pili maisha yao ni mazuri, ni yenye furaha, amani na upendo bila kujua kuwa hata wao walipitia nyakati za ugomvi, malumbano na mikwaruzano, lakini mwisho wa siku wakavumiliana, wakafikia hapo ambapo wewe unaona wamefika.

Ndoa inahitaji uvumilivu wa hali ya juu, si kwa mwanamke au mwanaume, kwani vipindi vigumu na rahisi mnavipitia wote. Ni vyema mwanaume ambaye ni kichwa cha familia ukawa unampa taarifa mkeo au mwenza wako kuhusu kipindi ambacho unaona utakabiliana nacho siku zijazo.

Lakini ni lazima uwe makini na ujue namna ya uwasilishaji wa kile ambacho unataka kumjuza mwenza wako.

Katika uhalisia wa maisha, baadhi ya wanawake wamekuwa wakishindwa kuvumilia kwenye ndoa au uhusiano wao hasa wapenzi wao wanapokutana au kupitia vipindi vigumu.

Wengine hudiriki hata kutoroka au kutoa nafasi kwa mwanaume ambaye anahisi ana unafuu wa maisha, jambo ambalo haliwezekani kwa mwanaume huyo kuwa njema siku zote, hata yeye ana kipindi kigumu anachopitia ingawa namna ya kupita katika nyakati hizo zinatofautiana.

Unaweza kukimbia ndoa au familia yako kwa sababu ya kukosa kula kile unachokitaka, lakini ukaenda kukutana na mwanaume ambaye atakupa unachokitaka. Lakini maisha yako ya faragha yakawa ya shida. Kila unapokutana naye huna hisia zozote za kimapenzi juu yake.

Mapenzi hasa ya ndoa, yana changamoto nyingi sana, kikubwa ni kujua dhamira yenu kuwa mliungana kwa ajili ya kuishi siku zote hadi pale mmoja atakapotwaliwa na Mungu.

Mpenzi msomaji, kwa ushauri na maoni, tembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Ijumaa Wikienda, Insta:@mimi_na_uhusiano au jiunge na Mi&U kwenye WhatsApp kwa namba zilizopo hapo juu.

GABRIEL NG’OSHA

Leave A Reply