Siasa mpaka kitandani…! aibu yenu!

unhappy-couple-in-bedHII inaitwa ‘wiki ya lala salama’ kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumapili ijayo ya Oktoba 25. Naamini kila ulimi wa mtu unazungumzia siasa. Iwe kwa mapenzi ya dhati au kusikiasikia tu!Nasema kusikiasikia kwa sababu kuna watu wangu wa karibu nimebaini wanafuata mkumbo kwenye siasa.

Yaani wao si wanasiasa, wala hawaijui siasa, ila mdomoni wanavyobwabwaja utadhani wao ndiyo waheshimiwa.

Mada yangu ya leo inatokana na simu moja niliyopigiwa na msomaji mmoja akisema kuwa, ameoa. Huu ni mwaka wa nne sasa lakini mwaka huu, hasa kuanzia katikati, ndoa yake imekumbwa na sintofahamu.

Huyu bwana anasema kuwa, mke wake amekuwa akimwekea ngumu kumpa haki yake ya tendo la ndoa kisa ni kuwa na itikabdi mbili tofauti. Anasema yeye ni shabiki mkubwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo mkewe ni mfuasi mzuri wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao wanamuunga mkono mgombea wa Chadema.

Sasa kila anaporudi nyumbani hali inakuwa nzuri lakini ikifika muda wa kuangalia taarifa za habari saa moja na saa mbili usiku, mambo huanza kubadilika.

USHUHUDA WAKE
“Tukiwa tunaangalia taarifa ya habari hali inakuwa tete sana. Mvurugano mkubwa hutokea. Mke wangu si msemaji mzuri sana kama mimi ambaye nimejaliwa. Mgombea wangu akijaza nyomi nashangilia sana, wa kwake akijaza yeye hajui kushangilia. Sasa nikimtania kwamba mgombea wake hajajaza japokuwa amejaza ananuna.

SIASA KITANDANI
“Sasa mbaya zaidi, kununa kwake kunakwenda mpaka kitandani. Ikifika wakati nataka haki yangu ya nyumba, anasema amechoka. Lakini najua si kweli bali ananilipizia ili kunikomoa.

“Mpaka labda nimwambie mbona mgombea wake alijaza tena anakubalika ndiyo kidogo anaweza kubadili mawazo na kushiriki na mimi tendo la ndoa. Hii hali inanikera sana.”

KUNA HUYU
Haya, mbali na huyo, yuko msomaji wangu mwingine yeye anakaa Tangi Bovu, Mbezi, Dar es Salaam. Anasema tangu siasa ishike hatamu nchini, mume wake amekuwa akilala mzungu wa nne.

African couple having relationship problems, Cape Town, South AfricaAnasema: “Anko hii siasa afadhali uchaguzi upite ijulikane moja. Mimi mume wangu anagombea udiwani kupitia Chama cha ACT- Wazalendo. Nimekuwa nikimwambia hashindi kwani maeneo tunayoishi CCM ina nguvu sana, amekuwa akichukia.

“Tukifika kitandani usiku analala, ananipiga miguu. Nikimuuliza anasema hana mudi kwa sababu anahisi mimi namhujumu kwenye siasa wakati anajua mimi sina chama, bali namkubali mgombea mwenye sera za kuchapa kazi.”

WITO WANGU
Naamini mmesikia wote. Hii si sawa hata kidogo. Mimi naamini siasa ipo na wala haifungamani na maisha ya ndoa. Ndoa ni ndoa, siasa si ndoa japokuwa ina wapenzi wake.

Hekima inasema kama nyie ni wanandoa au wapenzi, mkajijua mna itikadi tofauti kuhusu siasa, basi mkiwa pamoja msijadili wala kuelekezana kuhusu siasa.
Ubaya wa siasa ni uleule ubaya wa ushabiki wa timu za mpira. Timu ya mmoja katika ndoa ikifungwa wala aliyefungwa hawezi kuhamia kwenye timu ya mwenzake. Kwa hiyo hakuna haja ya kuikosesha amani ndoa kisa siasa au kisa mpira.

Tena uzuri ni kwamba, wawili wakiwa pamoja na ili kujua mwenzako anapenda chama gani wala haina gharama. Hasa siku hizi za kampeni. Utamwona mwenzako ‘anavyoweweseka’ mgombea wake akimwaga sera.

Sasa kama wewe mgombea wa mwenzako si wako, ukiingiza neno la kejeli, tayari, kimenuka! Sasa kwa nini mfikie huko jamani? Kwa nini mharibu ndoa kisa siasa wakati wa kiapo wala kasisi au shehe hakuwauliza kama mtaambatana na kuwa kitu kimoja kwenye siasa!

Mimi naamini baada ya kupiga kura Jumapili ijayo, maisha yataendelea. Watoto wenu watataka mambo nje ya siasa. Hata jirani yenu atataka mambo nje ya siasa. Sasa kwa nini muipe nafasi kubwa kwenye uhusiano wenu?

Liangalieni hili kwa umakini wa hali ya juu ili kudumisha amani yenu ambayo kwa sehemu kubwa imemegwa na siasa.
Toa comment