The House of Favourite Newspapers

Siasa Mwaka Huu Vita Nzito!

0

Imelda Mtema

Nivita nzito! Wakati mtifuano wa mastaa wawili wa kike wa sinema za Kibongo ambao huko nyuma walikuwa wakipigia kampeni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Jacqueline Wolper Massawe na Aunt Ezekiel Grayson ukiwa umekolea, kumeibuka balaa lingine la mastaa wawili wa kiume wa tasnia hiyo, Jacob Steven ‘JB’ na Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ wanaodaiwa kuzichapa laivu.

 Staa wa filamu Bongo, Jacqueline Wolper Massawe.

AUNT AANIKA SIRI ZA WOLPER UKAWA

Katika sakata lao, Aunt anadaiwa kuanika siri za Wolper mara tu baada ya kung’atuka Ukawa akiwa na mwigizaji mwenzake, Vincent Kigosi ‘Ray’ ambao wamejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wakati anatimkia CCM mapema wiki hii, Aunt aliliambia gazeti hili kuwa ameamua kuondoka Ukawa kwa kuwa sera za CCM zimemshawishi na kwamba mwanzoni alipotea na kwamba hahitaji mabadiliko badala yake anataka kuchapa kazi kama ilivyo kaulimbiu ya mgombea wa urais wa CCM, Dk. John Magufuli na kuiacha ile ya mabadiliko ya mgombea wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa.

Mara baada ya Aunt na Ray kutua CCM, ndipo kukaibukia maneno mitandaoni kwamba ni wasaliti, hali iliyosababisha Aunt kudaiwa kurushiana maneno makali na Wolper anayejiita Jacqueline Lowassa.Kufuatia hali hiyo kwenye mitandao hiyo ya kijamii, Aunt aliliambia Ijumaa kuwa anamshangaa Wolper kulivalia njuga suala lake la kuhamia CCM na kumwambia kuwa amehongwa.

Aunt Ezekiel Grayson.

“Jamani huyu mtu (Wolper) ananishangaza kupita kiasi, hivi inakuaje anahangaika na mambo yangu na kunisema nimehongwa fedha kuja CCM, basi na yeye aseme alitupa ngapi ili tujiunge Ukawa?” alihoji Aunt.

AUNT AMPA ONYO WOLPER

Aunt alisisitiza kuwa anamuomba Wolper kuacha kusambaza maneno ya kizushi kwa kuwa mwisho wa siku kila mtu atabeba mzigo wake mwenyewe hivyo aache kumfuatilia.“Mimi ningeomba sana aache kusemasema hovyo kwa sababu na yeye mbona hasemi ni kiasi gani alipewa kwa ajili ya kuja kutununua au anapenda kufuatilia tu mambo ya watu,” alisema Aunt

Staa huyo aliongeza kuwa Wolper akumbuke kuwa haya ni maisha tu ya uchaguzi na yanapita na pia kila mtu ana uhuru wa kuchagua wa kumpigia kampeni kama haridhishwi naye anaruhusiwa kuondoka pia.
“Jamani kwa nini mtu atumie muda mwingi kuumiza kichwa chake kwa ajili yangu? Wolper ajue kuna maisha baada ya uchaguzi na kila mtu ana uhuru wa kuchagua wapi aende na hata akikuta hakufai anaweza kuangalia kwingine,” alisema Aunt.

 Jacob Steven ‘JB.

Ijumaa licha ya kunasa maneno makali mtandaoni yaliyodaiwa ni kutoka kwa Wolper kwenda kwa Aunt, lilimtafuta tena kuzungumzia vita yake hiyo na mwenzake ambapo safari hii alionekana kuwa mpole kwa kusema kwa kifupi: “Nitakapotulia ndipo nitalizungumzia hilo.”

JB, Steve Nyerere wazichapa

Kwa upande wao JB na Steve Nyerere, Waandishi Wetu walinyetishiwa kuwa walizinguana na kufikia hatua kukunjana na kuchapana mapema wiki hii kwenye Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar baada ya kupishana kauli.
Chanzo makini kilichokuwepo eneo la tukio kilidai kuwa, awali mastaa hao walikuwa wamekaa pamoja wakiburudika na kupiga stori mbalimbali kabla ya mambo kwenda mrama.

Mnyetishaji wetu alizidi kudai kuwa baada ya muda mfupi, Steve Nyerere alianza kurusha madongo kuwa wasanii wanadai ni CCM damu lakini hawaweki kitu chochote mtandaoni kinachohusiana na chama hicho, akimsisitizia JB kuwa amekuwa akimsema kwa watu.

Chanzo kilisema kuwa kitendo cha Steve kumwambia maneno hayo JB, msanii huyo alijaribu kumuomba amtajie ni maneno gani ambayo alimsema kwa watu lakini Steve hakumjibu zaidi ya kuendelea kurusha maneno.
“JB alikuwa akimsihi sana Steve amwambie alimsema nini kwa watu na ni maneno gani lakini hakumwambia zaidi tu ya kurusha madongo yasiyo na idadi,” kilidai chanzo hicho.

Steven Mengere ‘Steve Nyerere’.

Mpashaji wetu huyo alitiririka kuwa kitendo cha Steve kuendelea kuzungumza kilimpandisha hasira JB ambaye alijikuta akipindua meza na kwenda moja kwa moja kumkunja Steve na kumzibua huku naye akijaribu kujibu mapigo.
Alisema kuwa baada ya kushikana na kuleteana songombingo, ilibidi Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda aliyekuwepo maeneo hayo kuamulia ugomvi huo ambao ulishaanza kukusanya ‘inzi’.

STEVE ANENA!

Baada ya kupata taarifa hizo, gazeti hili lilimtafuta Steve ambaye alikiri kutokea kwa tafrani hiyo lakini akaweka wazi kuwa walimalizana.Kwa upande wake JB, simu yake ya mkononi haikuwa inapatikana hadi gazeti hili linakwenda mitamboni.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply