The House of Favourite Newspapers

Sijamuelewa Waziri Kairuki na Sifa ya ‘Kujua Kusoma na Kuandika tu’

0

NA WALUSANGA NDAKI | UWAZI | NIONAVYO MIMI

HATIMAYE minong’ono, manung’uniko na wasiwasi kuhusu uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma, vilifikia kilele, Ijumaa ya wiki iliyopita ambapo Rais Dk. John Pombe Magufuli alikabidhiwa taarifa ya suala hilo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki (pichani).

Ripoti hiyo iliyofanyiwa kazi nchi nzima, ilibaini kuwa, watumishi 9,932 walighushi vyeti na kupata nafasi walizokuwa wamezishika sehemu mbalimbali nchini huku wakipata mishahara iliyoonekana kwa nje kuwa ni halali.

MABILIONI YA MISHAHARA YAMELIPWA

Kwa mahesabu ya ‘harakaharaka’, watu hao kama kila mmojawapo alikuwa akilipwa angalau kiasi kidogo tu cha mshahara wa Sh. 300,000 (laki tatu) kwa mwezi, kwa mwaka serikali ilikuwa inalipa wafanyakazi feki Sh. 35.7 bilioni!

Hicho ni kiasi kikubwa cha fedha ambacho wajanja hao walikuwa wanakipata kwa njia za ulaghai kupitia uovu wao binafsi au kwa kusaidiwa na watu wengine waliokuwa katika ofisi za umma.

UHAKIKI WA KIHISTORIA

Hatua ya kupambana na uovu huo iliyofanywa na uongozi wa sasa wa awamu ya tano inastahili pongezi zisizopimika kwani haijawahi kufanywa kitaifa nchini na utawala wowote tangu tupate uhuru mwaka 1961.

Kitendo hicho kilichofanywa na uongozi wa Rais Magufuli ni moja ya dhamira za kuonesha umakini wake kama alivyofichua maelfu ya majina ya watumishi hewa ambayo ‘wajanja’ wa nchi hii walikuwa wakiyatumia kujaza mifuko na matumbo yao kwa miaka nendarudi bila ya kuwa na aibu wala woga!

Hata hivyo, pamoja na wananchi wema kuungana na kuipongeza dhamira hiyo ya serikali, bado wanaona kuna haja ya moto huo wa kufichua vyeti feki ufike katika kila kona ya watu wote wenye dhamana ya kusimamia na kuongoza maisha na masilahi ya Watanzania wenzao.

Rais Dkt. John Magufuli akipokea Ripoti ya Uhakiki wa Vyeti vya Watumishi wa Umma.

KAULI YA KAIRUKI YATIBUA

Kauli iliyotolewa na waziri mwenye dhamana, Angellah Kairuki kwamba uhakiki huo haukuwahusu wanasiasa, mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wabunge kwa kuwa sifa za kuteuliwa kwao ni KUJUA KUSOMA NA KUANDIKA TU, imeacha wimbi la sintofahamu kwa wananchi ambapo walitegemea zoezi hilo la kuhakiki uhalali na uadilifu kwa watumishi wote wa umma lingewakumba pia viongozi hao.

Kivitendo, nafasi za viongozi hao ambao ‘wamenusurika’ chujio hilo ni muhimu na nyeti sana, kwani wao ndiyo wanyapara na viranja wakuu wanaosimamia wizara, mikoa, wilaya na idara zote zilizo chini yao, hivyo chujio la kuwagundua wadanganyifu na wenye kasoro katika nafasi zao lingepasa kuanzia kwao kabla ya wengine.

MADHARA KWA ‘WALIOPONA’

Kuwaacha viongozi hao bila kuwagusa kunamaanisha kuwaacha baadhi yao kama wapo katika nyumba za vioo. Hii inamaanisha kwamba hawatakuwa tena na uwezo wa kuwarushia wengine mawe ili kuwaweka sawa wakosefu walio chini yao. Hawatakuwa na uwezo huo wa kurusha mawe, kwani walengwa nao wanaweza kurusha mawe dhidi ya warushaji hao ambao eti katiba imewasaidia.

TEKNOLOJIA IMETUPITA

Si hivyo tu, sharti la kujua kusoma na kuandika tu kwa viongozi hao wakuu na wenye nguvu kubwa za kiutawala dhidi ya wataalam na wananchi wengine, haliendani na hali halisi ya matakwa ya jamii ya mwaka 2017!

Katika matakwa ya dunia ya leo ya teknolojia ya hali ya juu, viongozi hao ndiyo walitakiwa kuwa na sifa bora zaidi kuliko hata wataalam wetu, kwani wao ndiyo macho, masikio, mikono na kadhalika, vilivyo mstari wa mbele katika kuhakikisha ufanisi, usalama na furaha ya mamilioni ya wananchi walio chini yao.

BADO KAIRUKI ALIFUMBA

Kutohakiki usafi na uadilifu wa watu hao mbele ya jamii, kutaanza kujenga maradhi mabaya kwa wananchi kwamba mahali salama pekee pa kuweza kufanya kazi bila bugudha ya kudaiwa vyeti au kudhihirisha utaalam katika njia moja au nyingine, ni nafasi hizo za kuteuliwa ambazo masharti yake ni kujua kusoma na kuandika tu. Si hivyo tu, kwa bahati njema, Waziri Kairuki hakutaja hata kinachotakiwa kusomwa na kuandikwa tu ni nini!

Yote kwa yote, pamoja na kuipongeza dhamira hiyo ya utawala wa awamu ya tano kuhusiana na vyeti feki, kauli kwamba nafasi za mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya zinahitaji tu mtu awe na uwezo wa kusoma na kuandika, si kwamba inazishushia tu hadhi ofisi hizo muhimu zaidi nchini machoni mwa jamii, bali inatoa picha kwamba kazi nyepesi zaidi lakini zenye hadhi kubwa katika jamii ni hizo zilizotajwa.

VYETI FEKI SI KOSA LA JINAI?

Pamoja na mkanganyiko huo kuhusu viongozi hao, ukweli unabakia palepale kwamba suala la mwananchi yeyote kuwa na vyeti feki ni kosa la jinai awe na kazi za ofisini au akiwa anazurura mitaani!

Nionavyo mimi na ushauri wangu ni kwamba, uhakiki kwa viongozi wote ufanyike pamoja na hao wanasiasa, kwenye jinai asiwepo wa kupendelewa kwani hakuna aliye juu ya sheria katika nchi hii, vinginevyo, napata tabu kuamini kwamba tamko la Waziri Kairuki lilitoka kikinga zaidi kwa watu fulani jambo ambalo si sawasawa na kulaumiwa ni stahiki yake!

LIVE: Rais Magufuli Awatimua Kazi Watumishi 9,932 Wenye Vyeti Feki

Leave A Reply