The House of Favourite Newspapers

Siku 70 za Miss Tanzania lupango!

0

shose snari (1)Miss Tanzania Mwaka 1996 na aliyekuwa mkurugenzi kwenye Benki ya Stanbic, Shose Mori Sinare.

Ojuku Abraham, Amani

DAR ES SALAAM: Leo ni siku ya 70 tangu Miss Tanzania Mwaka 1996, Shose Mori Sinare aanze kusota lupango katika Gereza la Ukonga jijini Dar akikabiliwa na mashtaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, maisha yake yaanikwa na Amani linakupa zaidi.

shose snari (2)Miss Tanzania Mwaka 1996, Shose Mori Sinare (katikati).

TUHUMA ZAKE

Shose, aliyekuwa mkurugenzi kwenye Benki ya Stanbic, anashtakiwa pamoja na wengine wawili, kamishna mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na Sioi Graham Solomon aliyekuwa ofisa mwandamizi wa zamani wa taasisi hiyo ya fedha.

ANAVYOHENYA

Katika siku zote hizo, Shose amekuwa akihenya kupata dhamana, lakini inashindikana kutokana na kuwepo kwa kosa la utakatishaji fedha, ambalo kisheria halina dhamana.

Licha ya kosa hilo la utakatishaji fedha, mashtaka mengine yanayomkabili Shose ni pamoja na kudaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo kwa lengo la kujipatia fedha, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, makosa ambayo yote anadaiwa kuyafanya alipokuwa mfanyakazi wa benki hiyo ambapo nyakati tofauti, wote wanatuhumiwa kujipatia kiasi cha dola milioni 6 (sawa na shilingi bilioni 13) kutokana na mkopo wa serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard ya Uingereza wa dola milioni 600 (sawa na shilingi trilioni 1.3).

CHANZO KUTOKA GEREZANI

Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka gereza alipo Shose, amekuwa akisali usiku na mchana kumwomba Mungu awe upande wake.

“Kinachomuumiza sana ni ile nenda rudi ya mahakamani. Yeye hakuzoea misukosuko. Kwa hiyo anahisi kuchanganyikiwa na hali hiyo inampa tabu sana.

“Wakati mwingine anashangaa kuona kama siku haziendi vile, si unajua mambo ya kesi. Kwa kweli uchangamfu wake ni wa usoni tu lakini ndani ya moyo anaumia sana yule mrembo.

“Ila naweza kusema kwamba, ndugu zake wanampa sapoti kubwa kwani huwa wanakuja kumuona. Kilio chake kikubwa Shose ni kupata dhamana, hilo ndilo analoliombea kwa Mungu. Lakini vinginevyo ni mdada mtulivu sana, si mwongeaji akiwa mahabusu na wenzake. Anaonekana ana akili sana.

“Siku moja nilimuuliza anajisikiaje kuwa mahabusu akasema ni changamoto za maisha ambazo binadamu hupitia, siku za mwanzo, yaani ile siku ya kwanza, ya pili na ya tatu, zilikuwa ngumu sana kwake, lakini baadaye akakubaliana na hali halisi,” kilisema chanzo hicho.

WAREMBO WAMWOMBEA

Baadhi ya washiriki na washindi waliopata kutwaa taji hilo kwa miaka tofauti, walimuombea kwa Mungu, Shose  ili kesi hiyo yenye ushindani mkubwa wa kisheria, iweze kumalizika salama kwa upande wake.

“Dunia ina mapito mengi na hii yote ni mitihani ambayo mwisho wa siku tunamtegemea Mungu kuweza kushinda. Kesi ni kesi, lolote linaweza kutokea, lakini Mungu ni mkubwa, tunamuombea,” alisema mshiriki wa Miss Tanzania 2001, Rashida Wanjara…

Naye Miss Tanzania 1999, Hoyce Temu kwa upande wake, alisema amekuwa akimwombea kwa Mungu mrembo huyo kuhusu kesi yake.

“Najua ishu ipo mahakamani na bado hukumu haijapita. Kwa hiyo ni mtuhumiwa tu hajapatikana na hatia. Watanzania tumwombee Shose (pichani) kwani yaliyompata ni changamoto za dunia kama mwanadamu,” alisema Hoyce.

TUJIKUMBUSHE

Shose aliyeshinda taji hilo akichukua mikoba ya Emily Adolf, alikuwa mlimbwende aliyetoa matumaini makubwa ya kushinda Miss World, hasa kutokana na uwezo wake mkubwa katika lugha ya Kiingereza, ambayo wakati huo ilionekana kuwa tatizo lililowaangusha watangulizi wake.

Hata hivyo, kama walivyokuwa washindi wote wa taji la Miss Tanzania, ukimuondoa Nancy Sumari walioshiriki shindano la dunia, Shose hakufanya vizuri kwenye michuano hiyo ambayo mwaka huo ilifanyika Bangalore, nchini India na Miss Ugiriki, Irene Skliva kutwaa taji.

Leave A Reply