The House of Favourite Newspapers

Siku Zote Global Tunasimamia Ukweli

0

MARA kadhaa Kampuni ya Global Publishers, wachapishaji wa Magazeti ya Ijumaa Wikienda, Uwazi, Risasi Mchanganyiko, Risasi Jumamosi, Amani, Ijumaa na Championi, tumekuwa tukieleza namna ambavyo habari zetu siku zote husimamia ukweli tupu.

 

Kuandika uongo au habari za kumuonea mtu kwa uzushi wa jambo lisilo na ukweli, kwetu ni mwiko. Kama kinavyojieleza kichwa cha tamko hili, tunalazimika kufafanua juu ya habari zetu ambazo mara nyingi kuna watu ambao huwa wanatumia nguvu kubwa kusema habari fulani inayoandikwa na Magazeti ya Global ni ya uongo.

 

Hatujui huwa lengo lao ni lipi kwani mara zote huwa hawana sababu, hoja au ukweli juu ya habari husika! Jambo hili la kuambiwa kuwa habari zetu ni za uongo bila mtu kueleza kwa nini anaamini kuwa habari hiyo ni ya uongo, limekuwa likitukwaza mno na hasa pale tunapokuwa na ushahidi wote juu ya habari husika na kuuanika kwa kuambatanisha na habari hiyo.

 

Lakini wale wanaojifanya wataalam wa kutoa maoni mitandaoni huishia kusema tu ni habari ya uongo kwa kuwa wana vidole vya kuandika maoni na Mungu amewajalia kujua kusoma na kuandika. Inaudhi na kukera sana! Ieleweke kuwa, Global haichapishi habari yoyote isiyokuwa na ushahidi.

 

Tunatambua kwamba mbali na kulipishwa fidia baada ya mhusika kutushtaki na kushinda mahakamani, tunaweza kuchukuliwa hatua nyingine kali za kisheria zikiwemo hata za kufungiwa gazeti. Hivyo kila habari tunayoipata lazima tujiridhishe kwa kina kabla ya kuichapisha.

 

Tunajiuliza, kwa yeyote anayesema habari zetu ni za uongo, kwa nini asituchukulie hatua stahiki ikiwemo kutufikisha mahakamani au mamlaka nyingine zinazostahili? Tunayo mifano mingi ya habari ambazo mara nyingi tukishaziandika na kwa kuwa anayeandikwa ana wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii, basi huishia kudai kuwa ni habari za uongo, lakini wanapotakiwa kwenda kwenye vyombo vya kisheria ili kupata haki zao, huingia mitini au kuomba yaishe kwa maelezo kuwa walikanusha ili ‘kuua soo’ lakini habari ni ya ukweli mtupu.

 

Hivyo kwa maelezo hayo, kwa yeyote anayedai kuandikwa habari za uongo na Magazeti ya Global, basi amwage ushahidi au aende mahakamani au kwenye vyombo vingine vya kusimamia tasnia ya habari ikiwemo Baraza la Habari Tanzania (MCT) au kwa Waziri wa Habari, nasi tupo tayari kumlipa fidia.

 

Lakini ukweli ni kwamba tumechoshwa na watu ambao mara zote husema kuwa habari zetu ni za uongo bila kuwa na ushahidi wowote ilimradi tu kutuaribia sifa njema ya kuwahabarisha watu wetu tuliyojijengea. Tuache roho chafu za namna hiyo! Mungu ibariki Tanzania! Nawasilisha, Sifael Paul –Mhariri Global Publishers

Leave A Reply