MPIGA Picha Mkuu wa Kampuni ya Global Publishers wachapishaji wa Magazeti ya Uwazi, Ijumaa, Risasi, Ijumaa Wikienda, Amani, Championi, Spoti Xtra na Betika, Richard Bukos amepata pigo kubwa kwa kuondokewa na kaka yake, Samson Bukos aliyefariki dunia juzi, Alhamisi, Machi 21, mwaka huu katika Hospitali ya Amana, jijini Dar es Salaam.
Mwili wa Samson umezikwa leo, Jumamosi, Machi 23, 2019 katika makaburi ya Mburahati jijini Dar es Salaam ambapo wafanyakazi wa Kampuni ya Global Publishers wakiongozwa na Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Abdallah Mrisho wameungana na ndugu, jamaa, marafiki na waombolezaji wengine kuwafariji wanafamilia ya Bukos, nyumbani kwao, Kigogo Ruhanga.
Wakati wa kuaga mwili wa Samson, simanzi, majonzi, na vilio vimetawala kwa ndugu na watu wa karibu wa marehemu kutokana na ukaribu waliokuwa nao kwa ndugu yao huyo ambaye amefariki ghafla baada ya kuugua kwa muda mfupi hali iliyosababisha mama wa marehemu kuishiwa nguvu.
Aidha, katika ibada fupi ya kuaga na mazishi ya mwili wa marehemu, iliyoongozwa na Mchungaji Hasheem Atilio wa Nazareth Miracle Church amesema kuwa Samson Bukos amepumzika na waliobaki wanapaswa kumrudia Mungu na kutenda mema ya kumpendeza Mungu angali wakiwa hai kwani siku ya mwisho kila mwanadamu atahukumiwa kulingana na matendo yake.
“Ni heri kumkumbuka Mungu ukiwa baa unakunywa bia, kuliko kumkumbuka mchepuko wako wakati ukiwa kanisani kwenye ibada,” amesema Mchungaji Atilio.
Pia, mchungaji huyo ameitaka familia ya Bukos kutohuzunika sana kwani marehemu alimwamini Mungu, hivyo wamuombee ili Mwenyezi Mungu ampokee peponi.
PICHA NA DENIS MTIMA | GLOBAL PUBLISHRERS
Comments are closed.