The House of Favourite Newspapers

SIMANZI NZITO MGODINI

NI simanzi nzito! Wachimbaji wawili wa dhahabu katika Kijiji cha Izumbi, Sangamba Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wamefariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo katika Mgodi wa Mwembe wilayani Chunya, Mbeya. 

 

Tukio hilo la kusikitisha lilijiri Julai 2, mwaka huu, majira ya saa 10:00 jioni ambapo wachimbaji hao walipoteza maisha baada ya kuangukiwa na kifusi kilichochanganyika na mawe.

 

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Lusekelo Lwesya aliliambia gazetio hili kuwa alipata taarifa ya tukio kutoka kutoka kwa Balozi wa Nyumba Kumi, Hamis Mkumbo.Aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Zakayo Zablon Myunga (30) na Ayoub Nelson (33) katika mgodi huo unaomilikiwa na Mwembe Msemakweli.

 

Alisema kuwa, baada ya kupata taarifa hizo alitoa taarifa kwa mtendaji wa kijiji hicho, Flora Noel Chiwanga. Alisema baada ya hapo walipiga mbiu kuomba msaada kutoka kwa wananchi ambao walifanya juhudi za kuwaokoa umbali wa mita arobaini na tano kutoka juu ambapo waliwakuta majira ya saa mbili usiku wakiwa wameshapoteza maisha.

Alisema baada ya hapo walipelekwa katika Zahanati ya Kijiji cha Sangamba ndipo ikathibitishwa na mganga mfawidhi kuwa wote walikuwa wameshapoteza maisha. Mtendaji wa Kata ya Sangamba, Ntundu Chapa alitoa taatifa polisi ambapo walifika eneo la tukio kisha kwa kushirikiana na daktari waliifanyia uchunguzi miili ya marehemu na kuwakabidhi ndugu kwa ajili ya mazishi.

Anna John Mwailondele (26) ni mke wa marehemu Zakayo ambaye aliliambia gazeti hili kuwa wakati wa tukio yeye alikuwa kwenye shughuli zake ndipo alipopata taarifa za mumewe kufukiwa kwenye mgodi. Alisema yeye na Zakayo wamejaliwa kupata watoto wawili.

 

Kwa upande wake, Mwiteni Mwashiuya (30) ambaye ni mke wa Ayoub alisema mumewe alimuaga anakwenda kazini kuchimba, lakini ilipofika jioni alipata taarifa kuwa mumewe ni miongoni mwa waliofukiwa na kushuhudia mwili wake ukitolewa mgodini.

 

Hili ni tukio la pili kutokea katika Kata ya Sangambi la watu kufa kwa kufukiwa na kifusi kwenye machimbo hayo ya dhahabu. Tukio la awali lilitokea mwezi Machi, mwaka huu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Ulrich Matei alithitisha kutokea kwa tukio hilo na kutoa rai kwa wamiliki wa migodi kuzingatia sheria za usalama kazini.

 

Matei alisema chanzo cha vifo hivyo ni kukosa hewa pia na kujeruhiwa na mawe kichwani na maeneo mbalimbali ya miili yao. Hata hivyo, alisema Jeshi la Polisi linaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali kama Osha wanaotoa elimu ya usalama mahali pa kazi.

Comments are closed.