The House of Favourite Newspapers

Simba Bingwa, Yaweka Rekodi Kama Liverpool

0

UWANJA wa Sokoine uliopo jijini Mbeya, leo kazi ni moja kwa Simba kucheza mbele ya wenyeji wao, Prisons huku wakiwa tayari ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.Ubingwa wa Simba ni rekodi kama ilivyokuwa kwa Liverpool ilivyotwaa Premier msimu huu kwani zote zimejihakikishia ubingwa bila ya kushuka dimbani.

Wakati kule England Man City ikifungwa na Chelsea mabao 2-1 na Liverpool kutangaza ubingwa wakiwa maskani wametulia, Simba nao jana ilikuwa kama hivyo, wametangaza ubingwa wakiwa wanapiga stori wakati Azam ikitoka sare ya bao 1-1 na Biashara United, huku Yanga wakiichapa Ndanda mabao 3-2.

 

Ushindi wa Yanga unaweza usiwe na maana kubwa kwani katika mechi sita ilizobaki nazo, ikishinda zote ndiyo inafikia pointi za sasa za Simba, lakini katika uwiano wa mabao imeachwa mbali. Yanga ina tofauti ya mabao 13, wakati Simba ina 56.

Kwa Azam ikiwa nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi 59, mechi sita ilizosalia nazo ikishinda zote itakuwa na pointi 77 ambazo Simba imezivuka.Turudi kwenye mchezo wa leo; Kwa sasa Simba na Prisons wote wakiwa wamecheza mechi 31, Simba wana pointi 78, huku Prisons wakiwa na 42.

 

Simba ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck, itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kuichapa Mbeya City mabao 2-0, Jumatano iliyopita, huku Prisons chini ya Kocha Adolf Rishard, ikitoka kulazimishwa sare ya 2-2 na JKT Tanzania. Mechi hizo zote zilichezwa Uwanja wa Sokoine.

 

SHEREHE ZA UBINGWA SASA

Habari zinaeleza kuwa, mabingwa hao watetezi tayari wameshaanza kujipanga kwa ajili ya shangwe la ubingwa ambapo wachezaji pamoja na benchi la ufundi wametengewa fungu nono kwa kila mmoja kupata zaidi ya Sh milioni 10.Mbali na hilo, kuna tisheti maalum za kushangilia ubingwa huo zimesha andaliwa ambapo baada ya mchezo kumalizika leo, basi wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi watazunguka nazo uwanjani kushangilia pamoja na mashabiki wao ambao Serikali jana iliruhusu waingie kushuhudia mtanange huo.

Baada ya kurudi Dar, kuna mapokezi makubwa wameandaliwa na mashabiki na wanachama wa klabu hiyo katika kuwapongeza kwa kazi kubwa waliyoifanya msimu huu. Akizungumza na Spoti Xtra, Katibu wa Simba, Arnold Kashembe, alisema kuna mpango maalumu ambao upo kwenye uongozi na ukikamilika utawekwa hadharani.

 

“Zawadi ni jambo ambalo linatarajiwa kufanyika, tukikamilisha michakato yetu kila kitu kitawekwa sawa,” alisema katibu huyo.

 

TAJI LA 21Simba hili ni taji lao la 21 la ligi hiyo, pia ni la tatu mfululizo. Ilitwaa msimu wa 2017/18, 2018/19 na msimu huu wa 2019/20.Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alisema kuwa wakiifunga Prisons, taji lao la tatu linawekwa kabatini jumlajumla.

 

Kauli hiyo ya Manara ilitiliwa mkazo na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo ambapo alisema: “Iwapo Simba itatwaa ubingwa wa ligi msimu huu, basi itakabidhiwa kombe hilo moja kwa moja na tutalazimika kutengeneza kombe lingine kulingana na sheria na kanuni jinsi ilivyo. Hilo kombe lingine litakuwa na viwango na la kuvutia zaidi kwa ajili ya msimu ujao.

 

”BALAA NDANI YA UWANJA

 

Mchezo wa leo utakuwa na ushindani mkubwa kwa kuwa inakuwa ni mara ya kwanza kwa Sven kukutana na Prisons inayonolewa na Adolf Rishard.Mchezo wa mzunguko wa kwanza wakati Simba ikilazimisha sare ya bila kufungana Uwanja wa Uhuru jijini Dar, Simba ilikuwa chini ya Kocha, Patrick Aussems raia wa Ubelgiji.

 

HESABU KICHWANI

Hesabu za Prisons ni kumaliza ligi ikiwa ndani ya tano bora na ili kufikia hatua hiyo ni lazima ishinde leo.Adolf anasema: “Tunahitaji kumaliza ligi tukiwa ndani ya tano bora na hatuwezi kufanikiwa ikiwa tutapoteza mchezo wetu dhidi ya Simba. Ni timu nzuri na ina mbinu nyingi, ila wachezaji wanatambua kazi yao.” Kwa upande wa Sven, anasema: “Lengo kubwa ni kuona tunatwaa ubingwa mapema, hilo linawezekana na wachezaji wanajua kwamba tunahitaji ushindi kwenye mechi zetu zilizobaki.

 

”ISHU YA KUKABIDHIWA KOMBE LEO

 

Uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), kupitia kwa Makamu Mwenyekiti, Steven Mguto, ameweka wazi kuwa kwa sasa bado hawajaanza mpango wa kuandaa kombe kwa kuwa ligi bado haijaisha.“Bado ligi haijaisha na bingwa hajajulikana bado, hivyo ni mpaka pale ligi itakapoisha tutajua tutalitolea wapi kombe hilo la ligi kuu, hivyo subirini, kila kitu kitangazwa.”

Leave A Reply