The House of Favourite Newspapers

Simba dakika 120, Yanga dakika 138

0

HAMISI-KIIZA-e1442762258493

Hamis Kiiza, Simba.

Omary Mdose na Kazija Thabiti, Zanzibar
KIKOSI cha Simba ambacho kipo visiwani hapa kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao wa kesho Jumamosi dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Yanga, kinaendelea kujifua vikali ili kuhakikisha kinawapa raha mashabiki wake siku hiyo.

Wakati Simba wakiwa Unguja, Yanga wao wapo Pemba na kazi ni ileile kujiandaa kuwaua Simba. Sasa Championi Ijumaa linakupa ripoti kamili ya kambi za timu hizo visiwani humo.

Timu hizo zinatarajiwa kukutana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambapo kumekuwa na tambo nyingi kutoka kila upande, hasa kwa kuwa zote zimeshinda mechi tatu za awali.
Katika mazoezi ya juzi na jana, Simba ilitumia dakika 120 kukamilisha programu zake kwenye Uwanja wa Amaan wakati Yanga ilitumia dakika 138 kukamilisha mazoezi kwenye Uwanja wa Gombani.

Simba ikiwa chini ya Kocha Dylan Kerr na msaidizi wake, Selemani Matola, walianza mazoezi saa 3:30 asubuhi na kumalizika saa 5:30 asubuhi.

Wachezaji wa Simba walionekana kuwa katika hali nzuri, waliokuwa majeruhi Jonas Mkude, Abdi Banda walishiriki katika progamu zote za mazoezi wakati beki Samir Nuhu ndiye pekee ambaye hakuwa fiti kutokana na kuonekana bado ana maumivu ya enka.

IMG_0352Simba ilianza mazoezi mepesi kisha wachezaji wakagawanywa makundi manne kuuchezea mpira, baadaye walifanya mazoezi ya viungo yaliyodumu kwa dakika 50.

Baada ya hapo, Kerr akawapanga mawinga, mabeki, viungo na washambuliaji huku akiwachanganya wale waliozoeleka kuonekana kwenye mechi za ligi na wale wanaoanzia benchi kwa lengo la kuwafanya wazoeane.

Katika zoezi hilo lililodumu kwa takriban dakika 30, mawinga na viungo walikuwa na kazi ya kutengeneza nafasi za kufunga kwa washambuliaji huku mabeki wakizuia.

Simba ilimaliza mazoezi kwa kucheza mechi ambapo wachezaji waligawanywa katika vikosi viwili bila kujali wanaocheza kikosi cha kwanza na wale wanaocheza cha pili.

Baada ya mazoezi, Kerr aliliambia gazeti hili: “Wachezaji wangu wote wana ari ya ushindi, ni Nuhu na Mohammed Fakhi ndiyo ambao bado hawapo fiti.”

Simba inatarajiwa kurejea jijini Dar, leo Ijumaa kama ambavyo Yanga nayo itarejea leo pia.
Upande wa Yanga, Kocha Hans van Der Pluijm, aliendelea na mazoezi kama kawaida, japokuwa ulinzi umekuwa mkali, kocha huyo ameonekana kuwa makini katika kila hatua, hakuna mwandishi ambaye aliruhusiwa kuzungumza na kocha wala mchezaji wa Yanga.

Leave A Reply