The House of Favourite Newspapers

Simba Day: Macho Yote Kwa Jamaa Hawa Leo

LEO Agosti 8, nje ya kuwa ni maadhimisho ya Siku ya Wakulima, kwa wapenzi wa soka hasa wale wa Simba ni sikukuu yao.

 

Kila mwaka inapofika Agosti 8, klabu hiyo huwa inahitimisha tamasha lao la Simba Day kwa timu yao kucheza mechi ya kirafiki.

Mara kadhaa mechi hizo zimekuwa zikichezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar kama ambavyo leo itavyokuwa ambapo Simba itacheza dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana.

 

Simba Day ilianzishwa mwaka 2009 na mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali ikiwa na lengo la kuwakutanisha wanachama, wapenzi na viongozi wa timu hiyo. Moja kati ya mambo ambayo hufanyika katika Tamasha la Simba Day ni kutambulisha nyota ambao watatumika kabla ya kuanza kwa msimu pamoja na kutambulisha  jezi zitakazotumiwa na timu hiyo kwa msimu husika.

 

Wakati Simba Day ya msimu uliopita, mashabiki wa Simba walikuwa na hamu kubwa ya kumuona Emmanuel Okwi akitambulishwa rasmi mbele yao baada ya kurejea kikosini hapo akitokea SC Villa ya Uganda.

Sio Okwi pekee, bali sura nyingi zilikuwa zikisubiriwa kutambulishwa mbele ya mashabiki wa Simba kama Aishi Manula na  John Bocco.

 

Lakini kwa Simba Day ya mwaka huu, kuna sura mpya nyingi ambazo mashabiki watataka kuziona na kusubiri nini ambacho watakifanya baada ya kujiunga na timu hiyo.

Kwa lugha nyepesi unaweza kusema mashabiki leo watakaojitokeza kwenye mchezo huu macho yote yatakuwa kwao, ambapo makala haya yanakupa juu ya orodha ya wachezaji ambao wataangaliwa kwa macho ya ukaribu zaidi.

 

Meddie Kagere

Wengi walianza kuona mbwembwe zake katika michuano ya Kagame Cup ambapo alifunga mabao manne katika mechi tano alizocheza.

 

Leo mashabiki wengi watamtazama kwa umakini wakitaka kuangalia kwa namna gani atacheza sambamba na washambuliaji wenzake, Emmanuel Okwi na John Bocco na pia kama ataendeleza moto wake ambao aliuonyesha katika Kagame.

 

Kagere amejiunga na Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya ambapo siku chache kabla ya kutua kwenye kikosi cha Simba, alifanikiwa kuinyanyasa timu hiyo zilipokutana katika michuano ya SportPesa Super Cup.

 

Hassan Dilunga

Huyu naye ni nyota mpya katika kikosi hiki. Ndiye mchezaji wa mwisho kabisa kusajilijiwa na kikosi hicho. Dilunga naye atakuwa na wakati mgumu wa kutazamwa kwa dakika 90 na mashabiki wakikaa kuona ni kitu gani atakiongeza katika kikosi chao kwenye idara ya kiungo ambayo ipo imara kwelikweli. Ikumbukwe kuwa Dilunga ndiye mchezaji bora wa michuano ya Kombe la FA msimu uliopita.

 

Chama Claytous

Mzambia huyu ambaye anasifika kwa pasi zenye macho, naye ni miongoni mwa wachezaji wachache ambao watatazamwa kwa ukaribu zaidi. Mashabiki watakua macho naye kwa sababu wanataka kuona hizo sifa anazopewa ni za kweli au ni maneno tu.

 

Pascal Wawa

Beki huyu kutoka Ivory Coast naye ni moja ya watu ambao ataingia machoni mwa mashabiki wengi wakitaka kumtazama juu ya kiwango chake ambacho wengi walikitilia shaka katika michuano ya Kagame Cup.

Mashabiki watakua wanamuangalia Wawa muda wote kuona kama amepanda kiwango chake au bado anatia wasiwasi. Kumbuka aliwahi kuichezea Azam na wakati huo alikuwa mlinzi imara kwenye kikosi cha timu hiyo.

 

Adam Salamba

Kubwa ambalo litawavuta mashabiki kumtazama katika mechi hii ni kutaka kuangalia namna ambayo ataweza kutoa changamoto kwa washambuliaji wenzake pale ambapo atapata nafasi ya kucheza.

Wengi watataka kuona ana kitu gani cha ziada kulinganisha na mastraika waliokuwepo kwa sasa ndani ya kikosi hicho kama Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na John Bocco.

 

Deogratius Munishi ‘Dida’

Zamani alikuwa mchezaji wa timu hiyo kabla ya kupitia timu zingine kadhaa ikiwemo Azam na Yanga.

Kwa msimu uliopita, Simba ilikuwa ikimtegemea zaidi Aishi Manula golini, huku Said Mohammed ‘Nduda’ na Emmanuel Mseja wakishindwa kutoa changamoto. Ujio wa Dida, mashabiki wa Simba watataka kuona anatoa changamoto gani kwa Manula na kwa kuanzia tu, katika mechi ya leo mashabiki hao watataka kuona uwezo wake zaidi licha ya awali kumuona kwenye Kagame Cup.

Comments are closed.