The House of Favourite Newspapers

Simba Haizuiliki CAF

0

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah Muhene ‘Try Again’ amesema kwa mikakati ya usiri kambini, umoja na ushirikiano uliopo, basi ngumu kutokea timu ya kuwazuia kufuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

 

Simba wameipata jeuri hiyo baada ya kukaa kileleni katika Kundi D wakikusanya pointi nne mbele ya ASEC Mimosas, RS Berkane na US Gendarmerie.

 

Akizungumza baada ya Simba kupata sare ya 1-1 ugenini dhidi ya US Gendarmarie, juzi Jumapili, Try Again alisema usiri mkubwa uliokuwepo kambini baada ya baadhi ya wachezaji kuugua ghafla, ulichangia kwa kiasi kikubwa wao kuambulia pointi moja ugenini.

 

Try Again alisema kabla ya mchezo huo, wachezaji wao akiwemo Jonas Mkude, aliugua ghafla, lakini hakuna mtu kutoka nje ya kambi hiyo ambaye alifahamu na kuwafanya wapinzani wakutane na sapraizi uwanjani.

 

“Haikuwa kazi rahisi kupata matokeo haya hapa ugenini, vijana wetu walipambana sana kutokana na kucheza katika mazingira magumu. “Moja ya ugumu tuliokutana nao ni hali ya hewa ambayo ilikuwa nzito iliyosababisha baadhi ya wachezaji wetu kuugua ghafla mara baada ya kutua hapa nchini.

 

“Pia mazingira ya hoteli zilizopo hapa nyingi za ovyo ikiwemo hii tuliyofikia, kwa mfano leo (juzi) siku nzima hakukuwa na maji hotelini, siyo hujuma, lakini hali ya kiuchumi hapa nchini ndiyo imesababisha haya yote, lakini tunashukuru hatujapoteza mechi.

 

“Hivi sasa nguvu na akili zetu tunazielekeza katika mchezo unaofuata dhidi ya Berkane, tayari tumeanza maandaliz hayo. “Mtendaji mkuu wetu Barbara (Gonzalez) ametangulia Morocco kwa ajili ya kuandaa mazingira ya kambi kwa maana ya hoteli tutakayofikia na uwanja tutakaoutumia mazoezini, usafiri na chakula.

 

“Hivyo tutakaa hapa Niger kwa siku mbili na baada ya hapo tutaanza safari kuelekea Morocco kwa ajili ya mchezo huo,” alisema Try Again.

 

Kwa upande wa Barbara Gonzalez, alisema: “Tayari tumekamilisha taratibu zote za maandalizi ya kikosi chetu kuelekea mchezo dhidi ya RS Berkane, tunajua ni mchezo mgumu lakini tuko tayari.” Inaelezwa kuwa, Barbara ameongozana na kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mzambia, Clatous Chama ambaye aliwahi kucheza Berkane kwa ajili ya kwenda kufanya umafia Morocco.

 

Naye Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco, amesema: “Tulijua ratiba ya michezo yetu hii miwili tangu mwanzo, hivyo tumefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha tunafanya vizuri, tutacheza na RS Berkane Februari 27, mwaka huu, tunajua hii ni miongoni mwa timu ngumu zaidi kwenye kundi letu.

 

“Lakini jambo zuri kwetu kuelekea mchezo huo ni kuwa ndani ya kikosi chetu tuna Clatous Chama ambaye amecheza Berkane na anaijua vizuri Ligi Kuu ya Morocco, hivyo atatusaidia kuelewa mazingira.”

WAANDISHI WETU

Leave A Reply