The House of Favourite Newspapers

SIMBA HII MPAKA MKOME

SIMBA hii itawapiga mpaka mkome kwani jana ilipata ushindi wa nne mfululizo bila kufungwa bao hata moja katika Ligi Kuu Bara baada ya kuifunga Majimaji ya Songea mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

 

Nahodha John Bocco ndiye aliyekuwa nyota wa mchezo huo kwani aliweza kuifungia Simba mabao mawili na kutengeneza moja na kuchangia kwa kiasi kikubwa ushindi huo wa nne mfululizo.

Chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Masoud Djuma, Simba huko nyuma iliifunga Ndanda FC mabao 2-0, ikaifunga Singida United mabao 4-0 halafu ikaifunga Kagera Sugar mabao 2-0, na jana walitupia tena nyingine 4-0 dhidi ya Majimaji.

 

Ndani ya mechi hizo nne, Simba imefunga mabao 12 huku ikiwa haijaruhusu bao hata moja na kupata pointi 12 ambazo sasa zimewafanya wajiimarishe kileleni na pointi 35.

Katika mechi hizo nne zilizoifanya Simba jumla kuwa imecheza mechi 15, Bocco amefunga mabao matano, Emmanuel Okwi ana manne, Shiza Kichuya, Said Ndema na Asante Kwasi wote wana bao moja moja.

 

Bocco aliyejiunga na Simba akitoka Azam FC mwanzoni mwa msimu huu, alidhihirisha ubora wake katika mchezo huo sambamba na Okwi.

Simba jana ilicheza kwa mara ya kwanza chini ya kocha wake mpya raia wa Ufaransa, Pierre Lachantre ambaye alisisitiza soka la kuachiana yaani marufuku kwa mchezaji kukaa na mpira muda mrefu.

 

Mfaransa huyo alitumia mfumo mpya wa 4-1-3-2 na kufanikiwa kutawala mchezo huo huku kikosi chake kikicheza soka la kuvutia na kufurahisha.

Katika mfumo huo, ilishuhudiwa James Kotei akianzia benchi lakini beki namba tatu Jamal Mwambeleko akaanzishwa kama winga namba saba.

Katika mchezo huo, dakika ya kwanza, Marcel Boniventure wa Majimaji alikosa bao la wazi akiwa karibu na kipa wa Simba, Aishi Manula ambapo mpira alioupiga uliokolewa na kipa huyo.

Simba nayo iliuanza mchezo huo kwa kasi ikitaka kupata bao la mapema lakini ukuta wa Majimaji ulikuwa makini kuondoa hatari zote.

 

Bocco aliifungia Simba bao la kwanza dakika ya 17 kwa kichwa akimalizia mpira uliorudi kwake baada ya kona ya Kichuya kuokolewa na mabeki wa Majimaji langoni mwa timu hiyo.

Kutokana na kulalamikia bao hilo, Jaffary Mohammed wa Majimaji alionyeshwa kadi ya njano na mwamuzi wa mchezo huo Erick Onoka wa Arusha.

Majimaji ikimtumia zaidi Peter Mapunda katika ushambuliaji, ilijitahidi kupambana kusawazisha bao hilo lakini jitihada zake ziliishia kwa mabeki Juuko Murshid na Erasto Nyoni wa Simba.

 

Bocco aliifungia Simba bao la pili kwa kichwa tena dakika ya 26 akiunganisha vizuri krosi ya Ndemla. Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili Simba iliingia kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la tatu dakika ya 52 mfungaji akiwa Okwi aliyemaliza mpira wa kona uliopigwa na Kichuya na kushindwa kuokolewa na mabeki wa Majimaji.

Okwi aliifungia Simba bao la nne dakika ya 68 akimalizia kazi nzuri ya Bocco aliyempigia krosi safi baada ya kuwatoka mabeki watatu wa Majimaji kwa kasi.

 

Licha ya baadaye kuwaingiza, Jerry Tegete na Six Mwasekaga, Majimaji chini ya Kocha Habib Kondo haikuweza kufurukuta mbele ya Simba iliyokuwa ikicheza soka la kasi na kuachiana mpira haraka.

Katika mchezo huo, Simba iliwatoa Jamal Mwambeleko, Juuko Murshid na Kichuya na nafasi zao wakaingia Mzamiru Yassin, James Kotei na Laudit Mavugo.

 

Majimaji iliyobaki na pointi 13 katika nafasi ya 14, wao waliwatoa Paulo Maona, Geoffrey Mlawa na Mapunda na nafasi zao wakaingia Alex Kondo, Mwasekaga na Tegete aliyewahi kucheza Yanga na Taifa Stars.

Katika mechi nyingine za jana, Singida ikiwa nyumbani iliwachapa Prisons bao 1-0 kwa bao la dakika ya 90 lililofungwa na Sumbi Elinyesi.

 Said Ally, Dar es Salaam

 

Global Publishers App imekurahisishia kutazama matokeo ya kidato cha nne kupitia simu ya mkononi. Install Global Publishers sasa uyasome yote: Bofya  au 

Comments are closed.