Simba Ijilaumu Yenyewe

SIMBA italazimika kujilaumu yenyewe baada ya kushindwa kutumbukiza wavuni mpira wa penalti dakika za nyongeza kipindi cha pili kupitia kwa nahodha John Bocco na kusababisha mchezo uishe suluhu dhidi ya Biashara.

 

Mechi hiyo kali, ilipigwa Uwanja wa Karume mjini Mara ambapo mechi hii ilikuwa ya kwanza kwa timu zote, mechi ijayo Simba atacheza ugenini dhidi ya Dodoma Jiji na Biashara atakipiga na Ruvu Shooting, mechi zote zitapigwa keshokutwa Ijumaa.

 

Turejee kwenye mechi ya jana; Mechi ilikuwa na kasi muda wote huku kila kikosi kikifanya jitihada za kusaka ushindi lakini ziliangushwa na umakini hafifu wa washambuliaji wao pindi walipoingia eneo la wapinzani.

 

Simba ambao mchawi wao mkubwa ni kushindwa kutumia nafasi za kufunga ilijikuta ikiendelea kukumbwa na hali hiyo jana ambapo beki wao, Israel Mwenda alishindwa kutupia kwani mashuti yake manne aliyopiga akiwa nje ya 18 yalikwama kwenye mikono ya kipa Biashara, James Ssetuba.

 

Ukiachana na huyo, pia Simba watajilaumu wenyewe kwa kushindwa kuwa watulivu ambapo safu ile ya ushambuliaji iliyokuwa inaongozwa na Meddie Kagere na Bocco.

 

Kagere alikosa nafasi ya wazi dk ya 33 pia ingizo jipya Duncan Nyoni alifanya jaribio dakika ya 76 ambalo liliokolewa na hata Peter Banda alikosa nafasi ya wazi akiwa na kipa dk 74.

 

Bocco hakuwa na bahati kwa kuwa penalti ambayo mwamuzi aliamua ipigwe kutokana na Pape Sakho kukatwa ndani ya 18 na kuzua utata kwa madai mchezaji wa Biashara alipiga takolini, alikosa na kufanya Simba wapoteze pointi mbili ugenini.

 

Pia nyota wa Biashara, Denis Nkane alikosa nafasi ya kufunga akiwa yeye na kipa Aishi Manula dakika ya 33 ambaye alitoka na kuudaka mpira.

 

MECHI ZINGINE

Kutoka Mbeya, Mwandishi Derick Lwayse anaripoti kuwa, mchezo kati ya Mbeya City na Prisons ambao ulikuwa na kasi ulishuhudiwa ukimalizika kwa wenyeji City kupata ushindi wa bao 1-0 lililofungwa ‘usiku’ na Peter Mapunda.

 

Huko jijini Dodoma, wenyeji Dodoma Jiji walipata alama tatu kwenye mchezo wao wa kwanza wa ligi dhidi ya Ruvu Shooting baada ya kuibandua bao 1-0 lililowekwa kimiani na Cleophace Mkandala dakika ya 33.

CAREEN OSCAR NA LUNYAMADZO MLYUKA


Toa comment