Simba Kukabidhiwa Ubingwa wa Ligi Kuu Julai 18
UONGOZI wa Simba, umeweka wazi kwamba utakabidhiwa ubingwa wao wa nne wa Ligi Kuu Bara katika mchezo dhidi ya Namungo FC utakaochezwa Julai 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.
Ikiwa itakuwa hivyo, basi itakuwa ni mara ya pili mfululizo Simba kutwaa ubingwa na kufanya sherehe mbele ya Namungo FC inayonolewa na Kocha Mkuu, Hemed Morocco kwa kuwa msimu uliopita wa 2019/20 ilikabidhiwa taji hilo Uwanja wa Majaliwa, Lindi wakati timu hizo zikimaliza mchezo bila ya kufungana.
Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema kuwa watapewa taji lao kwenye mechi yao ya mwisho.“Taji ni mechi ya mwisho (Namungo, Julai 18) kwa sababu mchezo wetu dhidi ya Azam FC tutacheza Uwanja wa Chamazi,” alisema Rweyemamu.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Karim Boimanda, alisema: “Bingwa hachagui mechi ambayo anahitaji kukabidhiwa ubingwa ila anaweza akaomba, Bodi ndiyo inapanga na kufanya maamuzi ya mwisho juu ya hilo. Kuhusu siku bingwa atakayotangazwa itatangazwa hivi karibuni.”