The House of Favourite Newspapers

Simba: Lazima Tupande Ndege, Leo ni Azam na Simba, Taifa

0
Wachezaji wa timu ya Simba na Yanga wakifanya yao.  

SIMBA iliyokuwa kambini Morogoro tangu Jumatatu wiki hii, imesema vyovyote iwavyo ni lazima msimu ujao ipande ndege kwa kushiriki michuano ya kimataifa na kwa kuanzia harakati zao wanaifunga Azam FC leo Jumamosi katika mechi ya Kombe la FA.

Kwa miaka mitano sasa, Simba haijafanikiwa kushiriki michuano ya kimataifa Afrika inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwani haikuweza kutwaa ubingwa au nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara ndani ya kipindi hicho.

Wachezaji wa Azam.

Makocha na wachezaji wa Simba, kwa pamoja wamepania kuifunga Azam leo katika nusu fainali ya Kombe la FA kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ili wafuzu kucheza fainali halafu watwae ubingwa.

 

Bingwa wa Kombe la FA anapata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo Simba inaamini ikiifunga Azam itafika fainali na kutwaa ubingwa kwa kucheza na ama Yanga au Mbao FC.

Hadi inafika nusu fainali katika Kombe la FA, Simba iliifunga Madini FC bao 1-0 katika robo fainali na Azam iliifunga Ndanda FC mabao 3-1.

Wachezaji wa timu ya Simba Sc.

Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja akizungumzia mchezo huo alisema: “Tunahitaji kushinda kwa hali yoyote ile ili tufike fainali na kutwaa ubingwa, tunataka kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.

“Tumewandaa wachezaji wetu katika eneo la kupiga penati iwapo itatokea tutamaliza dakika 90 bila ya kufungana au kuwa sare, ili kuweza kuwa fiti katika eneo hilo.”

Nahodha wa Simba, Jonas Mkude kwa upande wake alisema: “Mechi dhidi ya Azam huwa ngumu kwetu, lakini tutashinda na kufika fainali halafu ubingwa, tunataka tucheze mechi za Caf mwakani.

“Kukaa miaka mingi bila ya kushiriki mechi za kimataifa ni jambo ambalo linasikitisha, hivyo tutapambana kuona tunashinda mchezo huu.”

NGUVU YA YANGA

Simba itaomba Yanga itinge fainali kwani hata kama wao wakifungwa atakuwa na nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho endapo Yanga pia itatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Katika ligi kuu, Simba ipo kileleni na pointi 59 ikifuatiwa na Yanga yenye 56 na michezo miwili mkononi.  Bingwa wa ligi kuu anapata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

AZAM YATEMA CHECHE

Kocha wa Azam, Aristica Cioaba akizungumzia mchezo huo, alisema: “Tutajitahidi kupambana ili tuifunge Simba, kwani hii ndiyo michuano pekee inayoweza kutupa ubingwa na kupata tiketi ya mechi za Caf.”

Naye Nahodha Msaidizi wa Azam, Himid Mao alisema: “Tuna morali ya hali ya juu kuelekea mchezo huu, wachezaji wetu majeruhi wamerudi, tupo tayari kwa mapambano.”

 

Leave A Reply