The House of Favourite Newspapers

Simba: Mpeni Msuva Tuzo Yake

0
Kiungo wa Yanga, Simon Msuva.

NA OMARY MDOSE | CHAMPIONI | HABARI

KOCHA Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja raia wa Uganda, amesema katika mbio za kuwania Tuzo ya Mfungaji Bora Bara msimu huu, anaona kiungo wa Yanga, Simon Msuva ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuitwaa.

Mayanja amemtaja Msuva huku kiungo huyo akiwa ndiye kinara baada ya kufunga mabao 14 akifuatiwa na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting mwenye mabao 13, huku Mbaraka Yusuph wa Kagera Sugar na Obrey Chirwa kutoka Yanga wote wakiwa nayo 12. Takwimu hizo ni kabla ya mechi ya jana kati ya Yanga na Toto Africans. Akizungumza na Championi Jumatano, Mayanja alisema Msuva ana nafasi kubwa ya kuchukua tuzo hiyo kutokana na kujituma kwake uwanjani huku pia akiwa na uwezo wa kufunga mabao kwa njia yoyote ile.

Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja raia wa Uganda.

“Ushindani mkubwa uliokuwepo msimu huu umesababisha washambuliaji wengi kufunga mabao machache kuliko msimu uliopita ambapo kinara alimaliza ligi akiwa na mabao 21, ukiangalia kwa sasa hali jinsi ilivyo, hakuna atakayeweza kufikia mabao hayo.

“Lakini ushindani wa kuwania tuzo ya ufungaji bora unaonekana kuwa ni mkali kwani ukiangalia orodha yao utagundua kuna wachezaji kama wanne wanaoshindania tuzo hiyo, lakini kwa upande wangu naona Msuva ana nafasi kubwa ya kuwa mfungaji bora msimu huu.

“Nasema hivyo kwa sababu ana uwezo wa kufunga kwa kichwa pamoja na kutumia miguu yote, lakini hata yule straika wa Ruvu Shooting (Abdulrahman Mussa), naye anakuja vizuri, hivyo Msuva nampa nafasi ya kwanza akifuatiwa na huyo wa Ruvu Shooting, nafikiri mwisho atapewa tu tuzo yake,” alisema Mayanja. Ikumbukwe kuwa, msimu uliopita, Amissi Tambwe wa Yanga ndiye aliyeibuka kinara wa ufungaji akifunga mabao 21, akifuatiwa na Hamis Kiiza aliyekuwa akiichezea Simba na kufunga mabao 19.

Leave A Reply