Simba na Dodoma Jiji Kukiwasha leo Dodoma

SIMBA SC, leo wakitarajiwa kuvaana na wenyeji wao Dodoma Jiji FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara, wameamua kwenda na mziki wa maana wenye wachezaji 20.Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, leo Alhamisi watakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kupambana na wenyeji wao hao ukiwa ni mchezo wa kiporo.

 

Kila timu leo itahitaji ushindi kama kuweka heshima jambo ambalo linaufanya mchezo huo kuwa wa kibabe.Simba yenye pointi 35 katika msimamo wa ligi ikishika nafasi ya pili, itapambana na Dodoma iliyokusanya pointi 22 ikiwa nafasi ya kumi.

Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Simba, Abass Ally, ameweka wazi kuwa, wamelazimika kusafiri na kikosi cha wachezaji 20, huku wengine wakibaki jijini Dar es Salaam wakiendelea na program za mazoezi walizopewa na kocha wao raia wa Ufaransa, Didier Gomes Da Rosa.

 

Miongoni mwa wachezaji walioachwa jijini Dar, ni Erasto Nyoni, Junior Lukosa raia wa Nigeria na Peter Muduhwa raia wa Zimbabwe.“Kwa jumla kikosi cha wachezaji 20 tulichosafiri nacho kiko salama na kwamba, tupo tayari kwa ajili ya mchezo dhidi ya Dodoma FC.

 

“Kwa jumla kocha Didier Gomes ametuhakikishia ushindi kwenye mchezo huo, hivyo amewaomba mashabiki wote kuisapoti timu kwani ina kila sababu ya kupata mtokeo mazuri na kutwaa pointi tatu huku ugenini,” alisema.

Kwa upande wa Kocha wa Dodoma Jiji FC, Mbwana Makata amesema kuwa, kikosi chake kina hatihati ya kuwakosa nyota wawili ambao ni Seif Karihe na Rajab Mgalula ambapo Mgalula anasumbuliwa na majeraha huku Karihe akiwa amechelewa kujiunga na kikosi kutokana na kuwa na matatizo ya kifamilia.

 

“Kikosi changu kiko vizuri licha ya kwamba kuna uwezekano wa kuwakosa wachezaji wawili, kubwa tumejiandaa kuvuna pointi tatu mbele ya Simba, tunaiheshimu ni timu nzuri sana ambayo ina wachezaji wenye maarifa mengi.

“Hivyo, tutahakikisha tunapigania kulinda rekodi yetu ya kutofungwa mchezo wowote katika uwanja wetu wa Jamhuri,” alisema Makata.

WATINGA BUNGENI

Mapema jana asubuhi, msafara wa wachezaji wa Simba na viongozi wao, baada ya kutua Dodoma, walipata mwaliko wa kuhudhuria kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Wakiwa bungeni, wachezaji na viongozi wa Simba walipata muda wa kutambulishwa mbele ya wabunge jambo ambalo wengi walionekana kufurahia. Kisha baadaye wakapata muda wa kupiga picha ya pamoja nje ya bunge.

STORI NA MUSA MATEJA NA JOEL THOMASI, Dar es Salaam

⚫️ Kwa UPDATES zote, Download GLOBAL APP: ⚫️ ANDROID:http://bit.ly/38Lluc8 ⚫️ iOS:https://apple.co/38HjiCx

Toa comment