Simba nao wawatese waarabu Taifa, inawezekana

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa ngazi ya klabu, Simba kesho Jumanne watakuwa pale Uwanja wa Taifa wakitafuta pointi muhimu mbele ya Al Ahly ya Misri. Mchezo huo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni wa mzunguko wa nne na mpaka sasa hakuna timu ambayo ina uhakika wa kwenda robo fainali kwenye kundi lao.

Simba ipo Kundi D ikiwa na timu za Al Ahly iliyo kileleni na pointi zake saba, AS Vita ya DR Congo yenyewe ni ya pili ikiwa nazo pointi nne, halafu Simba ya tatu ikiwa na alama tatu na ya mwisho ni JS Saoura ya Algeria yenye mbili.

Simba imetoka kufungwa kwenye michezo miwili iliyopita kwa mabao 5-0 kila mechi, ilianza kufungwa na AS Vita kule DR Congo halafu ikapokea kipigo kama hicho kule Misri mbele ya Al Ahly ambao wanacheza nao kesho.

Sasa kesho Jumanne watakuwa wanaingia uwanjani kwa lengo la kusahihisha makosa yaliyojitokeza kwenye mechi mbili zilizopita kwa kuhakikisha wanapata ushindi utakaofufua matumaini zaidi ya kwenda robo fainali kisha hatua itakayofuata.
Siyo kazi ngumu kuwafunga Al Ahly kama kila upande utakuwa na mipango madhubuti ya kujitoa katika kila dakika watakapokuwa ndani ya uwanja.

Kama Al Ahly walishinda kwao basi Simba kesho na yenyewe inaweza kushinda nyumbani, hilo linawezekana kwa kiasi kikubwa na kwa kila mchezaji kuhakikisha analinda na kuitumia nafasi atakayopewa ya kucheza.

Angalia kama Simba iliwafunga Waarabu wa JS Saoura kutoka Algeria tena mabao 3-0 kwa nini ishindikane kwa Al Ahly? Hii inamaanisha kila mmoja anapambana nyumbani kwake kupata pointi, Simba wanatakiwa kutumia ‘formula’ hii.

Aidha mashabiki pia mnapaswa kujitokeza kwa wingi kutoa sapoti. Ukiangalia Simba katika mechi mbili zilizopita ilicheza ugenini bila mashabiki kama ilivyozoeleka wanapokuwa Taifa na kama walikuwepo basi ni wale wa kuhesabu sana, sasa wapo nyumbani ni vizuri kutumia fursa ya kuwa mchezaji wa 12.
Kila kitu kinawezekana ikiwa kila mmoja ana lengo la kutaka kufanikisha kitu fulani. Kila la heri Simba kuelekea kwenye mchezo huu muhimu.

Toa comment