The House of Favourite Newspapers

Simba Queens ‘The Galacticos’… Ndani Ntiti, nje Ntiti Yatawala ligi ya Wanawake

0
Simba Queens.
Simba Queens.

KWA miaka takribani minne sasa, kwenye soka la Wanawake Tanzania, kuna klabu moja tu ambayo imejiweka kwenye ukurasa wake wa tofauti.

Klabu hiyo ni Simba Queens. Timu hiyo imetawala ligi ya ndani kwa kutwaa mataji matatu ya ligi mfululizo. Kisha mwaka jana wakaenda kutengeneza ufalme wao Kanda ya Cecafa kwa kubeba ubingwa huo kwa mara ya kwanza kisha wakakata tiketi kwenda Ligi ya Mabingwa Afrika.

Huko nako hawakuwa wanyonge, walitinga nusu fainali ambako walitupwa nje na Mamelodi Sundowns, kisha bahati mbaya haikuwa kwao pia.

Walifungwa mchezo wa kumsaka mshindi wa tatu lakini waliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kufika hatua hiyo pia timu ya kwanza kwa Afrika Mashariki kufika hapo kwani Vihiga Queens ya Kenya ambao walikuwa wa kwanza kwenda CAF walitolewa kwenye makundi.

SABABU ZA MAFANIKIO

Mafanikio ya Simba hayakuja kwa bahati mbaya, waliijenga timu yao kwa miaka mitatu mfululizo, mwaka wanne wakaanza kuona matunda ya ujenzi wao.

Walianza kwa kujenga kikosi imara ambacho kilikusanya majina ya wachezaji bora wa ndani kwa asilimia 80 kutoka klabu za JKT Queens, Mlandizi Queens, Yanga na wachache kutoka nje ya Tanzania ikiwemo Burundi.

Hiyo ikawafanya wawe timu ya tofauti kidogo, taratibu wakaanza kuwanyang’anya utawala wa soka la Bongo, JKT Queens na hatimaye umekuwa wa kwao hadi sasa.

SIMBA QUEENS ‘THE GALACTICOS’

Galacticos ni jina ambalo lilikuwa linatumiwa na klabu ya Real Madrid kutoka Hispania, ambalo lilitokana na sera ya Rais wa timu hiyo, Florentino Pérez.

Sera ya Perez ilikuwa kununua wachezaji wa bei ghali na maarufu duniani. Ukiwatazama Simba Queens pia ni kama walikuwa wanapita kwenye hii sera bila wao kujua, msimu wao wa kwanza kwenye ligi, walimsajili Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’ kutoka Mlandizi Queens.

Wakati Mlandizi wanachukua ubingwa wa ligi kwa mara ya kwanza msimu wa 2016-17, yeye ndiye alikuwa staa, alifunga mabao 17 na kuwa mfungaji bora. Simba wakahamishia mabao hayo kwenye timu yao na ikawa usajili wa maana.

Kisha wakawavuta wachezaji wawili kutoka Burundi, Joele Bukuru na Asha Djafar ambao wakaja kuongeza kitu kikubwa kwenye timu hiyo.

Sera hiyo ikaendelea tena, kila msimu, wakamsajili Amina Bilal ‘Mido’ nahodha wa Yanga Princess kwa sasa kutoka Kigoma Sisterz ambaye alikuwa kiungo bora wakati huo msimu wa 2018-19, alionyesha zaidi ubora wake. Pamoja na Opah Clement ambaye naye alikuwa Kigoma.

BALAA LAO LILIKUJA HAPA

Msimu wa 2019-20, Simba walifanya kufuru haswa kwenye soko la usajili walichukua wachezaji bora wengi ambao walikuja kuwapa ubingwa, Fetty Densa, Zena Hamisi, Shelda Boniface, Maimuna Hamis ‘Mynaco’, Asha Kadosho na wengine wengi.

Msimu wa 2020-21, uchu wao wa kuongeza wachezaji wengi wa kigeni uliongezeka zaidi, wakaenda nje ya Afrika Mashariki, wakawashusha wachezaji wengi bora, Danai Bhobho wa Zimbabwe, Dorothy Mukatesha wa Zambia na Jeane Pouline wa Rwanda.

Msimu uliofuata, wakashusha vyuma kama Mawete Flaviana, Ruth Kipoyi hawa ni raia wa DR Congo, Merci Tagoe kutoka Ghana. Kisha wakamleta Pambani Kuzoya kutoka DR Congo pia.

Olaiya Barakat wa Nigeria, Philomena Abakha wa Ghana, Aquino Corozone, Ruth Ingosi na Jentrix Shikangwa wa Kenya, Watanzania Diana Mnali kutoka Fountain, Zainabu Mohamed kutoka Baobab Queens. Ester Mayala ambaye hakuwa na timu.

UREJEO WA GAUCHO, ONGEZEKO LA MWALALA

Ukitazama usajili wa Asha Rashid ‘Mwalala’ na Gaucho, siyo kwamba ulikuwa unahitajika sana ndani ya Simba, kikosi chao kilikuwa kinatosha kutetea ubingwa wao msimu huu.

Kilichotokea ni kama sera ya Galacticos inaendelea, kuwa na wachezaji bora na wenye majina, ingawa sasa, wachezaji hawa wanakwenda kuifanya Simba kuwa hatari zaidi ndani na nje ya uwanja.

MFANO WA KIKOSI KINACHOANZA

Kikosi cha kwanza Simba kinachoweza kuanza ni kipa Gelwa Yona, mabeki wakiwa Fetty Densa, Violet Nicklas na Ruth Ingosi kwa mfumo wa mabeki watatu.

Kisha viungo wakawa, Joele Bukuru, Aquino Corazone, Asha Djafar na Pambani Kuzoya. Mbele wakacheza, Mwalala, Opah na Gaucho. Kikosi cha pili; Janeth Shija, Diana Mnali, Dotto Tossy, Ester Mayala, Wema Richard, Koku Kipanga, Asha Mwinuka.

Jackline Shikangwa, Philomena Abakah, Olaiya Barakat. Kisha kwenye benchi kuna Zubeda Mgunda, Shelda Boniface, Silvia Thomas, Danai Bhobho, Carolyne Rufa na Lobo Bambadiala. Vikosi vyote hivi vinaweza kucheza na kuwapa ubingwa Simba.

Makala na Issa Liponda, Championi Jumatatu

Leave A Reply