Simba Sc Yaanza Vibaya Ligi Kuu

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba Sc wamekubali kubanwa mbavu na Wanajeshi wa mpakani, Biashara United baada ya kukubali sare ya bila kufungana katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu.

 

Mechi hiyo imepigwa katika Dimba la Karume mjini Musoma. Simba wamekosa nafasi ya dhahabu dakika za nyongeza baada ya kupata penati ambapo nahodha wao John Bocco amekosa penati hiyo. Simba wanagawana ponti moja moja na Biashara.

 

Katika mchezo huo ambao haukutawaliwa sana na ufundi pengine labda kwa sababu ya ubovu wa kiwanja, Simba hawakuonesha kile ambacho Mashabiki wao wamezoea kukiona katika mechi zao.

 

Ikumbukwe kuwa hii ni mechi ya tatu mfurulizo kwa Simba bila kupata bao lolote, kuanzia Mechi ya Simba Day waliofungwa bao 1-0 na TP Mazembe, mechi ya Yanga ya Ngao ya Jamii ambapo Simba aliambulia kichapo cha bao 1-0 na game ya leo ambayo wote wameambulia patupu.

 

Simba wamecheza mechi yao ya kwanza msimuu huu mpya wa 2021/2022 na wameanza kwa kudondosha alama mbili. Matokeo hayo huenda yakaleta presha kwa Mwalimu wa Kikosi hicho Mfaransa Didier Gomes.

Katika mchezo mwingine wa Ligi kuu Tanzania Bara, timu ya Mbeya City imefanikiwa kuibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Prisons, mfungaji wa goli akiwa ni Peter Mapunda 90+2′.

 


Toa comment