The House of Favourite Newspapers

Simba SC Ndege Lazima Aisee

0

NA Omary Mdose | CHAMPIONI| Dodoma

SIMBA imesema ni lazima iifunge Mbao FC leo Jumamosi katika mechi ya fainali ya Kombe la FA na kupata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Ikishiriki michuano hiyo, Simba itasafiri kwa ndege kwenda nchi mbalimbali kucheza mechi za Kombe la Shirikisho. Kwa miaka minne sasa Simba haijashiriki michuano ya kimataifa.

Mchezo huo wa fainali utakaochezeshwa na mwamuzi Ahmed Kikumbo kutoka Dodoma atakayesaidiwa na Mohammed Mkono wa Tanga na Omar Juma wa Dodoma, utachezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Hadi Simba inafika fainali iliifunga Azam FC bao 1-0 katika nusu fainali huku Mbao ikiifunga Yanga bao 1-0 katika hatua hiyo.

Akizungumzia mchezo huo wa fainali, Kocha wa Simba, Joseph Omog, raia wa Cameroon, alisema: “Fainali ni fainali, lolote linaweza kutokea, sisi tumejiandaa vizuri kuifunga Mbao, hatuwadharau kwa hapa walipofika, hivyo tutapambana nao kweli.”

Katika mchezo wa leo, Simba inatarajiwa kumkosa kiungo wake, Mohammed Ibrahim ‘Mo’ ambaye anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Azam. Pia Simba itamkosa beki wake, Hamad Juma ambaye ni majeruhi wa kidole cha mguu wa kushoto pamoja na Method Mwanjale ambaye kwa muda mrefu amekua nje.

Kocha wa Mbao FC, Mrundi, Ettiene Ndayiragije, akizungumzia mchezo huo alisema: “Kitendo tu cha kufika fainali ni mafanikio makubwa kwetu, hakuna aliyetarajia kama tutafika hapa.

“Uwezo wetu binafsi ndiyo umetusaidia na wala si bahati, tumeifunga Kagera Sugar kwa uwezo na hata Yanga nao tumewafunga kwa uwezo wetu, hivyo tunataka kuwafunga Simba ili kuweka rekodi.”

Kwa upande wa Mbao FC kikosi chao kipo kamili na hakuna hata mmoja aliyeripotiwa kuwa ni majeruhi wala mwenye adhabu.

Zajiandaa kwa penalti

Katika mazoezi yao ya mwisho waliyoyafanya kwenye Uwanja wa Jamhuri jana Ijumaa na juzi Alhamisi, timu hizo zilikuwa zikijifua katika kupiga penalti jambo ambalo linaashiria kwamba zinajiandaa kabisa kama zikifika hatua hiyo iwe rahisi kuibuka na ushindi.

Tiketi zaanza kuuzwa mapema

Jana Ijumaa, tiketi za mchezo huo zilianza kuuzwa kuanzia saa tatu asubuhi ambapo mashabiki wengi walijitokeza kwa ajili ya kuwahi nafasi. Viingilio vya mchezo huo ni; V.I.P A Sh 20,000, V.I.P B Sh 15,000 na mzunguko ni Sh 5,000.

 

Leave A Reply