Simba SC: Tunazuilika Na Naniii Kombe la Shirikisho

Wachezaji wa Simba wakiendelea na mazoezi.

 

SIMBA yenye rekodi za kipekee msimu huu nchini Tanzania, inarejea rasmi leo Jumapili kwenye Kombe la Shirikisho baada ya kuyakosa mashindano hayo tangu msimu wa 2012. Rekodi za Simba, zimeanza kuitisha Gendamarie ambayo baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere jana alfajiri walionekana kubabaika huku madereva Taxi wakidai kuwa wasipojipanga wataweka historia ya kipigo.

 

Sikia wanachojivunia Simba; Hawajawahi kupoteza mechi tangu ligi ianze, na wanashangaa mtu anafungwaje? Walioko ndani wale wa akiba wote ni moto kuanzia nyuma mpaka mbele.

Kipa wao namba moja, Aishi Manula hajui nini maana ya kupoteza mchezo, ameruhusu mabao machache kuliko kipa yoyote nchini. Sita tu.

 

Ukuta wake una mafundi; pembeni huku kulia kuna Shomari Kapombe kimataifa ndiyo mashindano yake. Analinda goli, anashambulia na kupiga krosi zenye macho. Mliona alichoifanya Kagera Sugar. Huku kushoto ndiyo patamu zaidi kuna mtu anaitwa Asante Kwasi, sifa zake ni kama za Kapombe lakini ni fundi wa kufunga.

 

Usimsahau beki bora wa Simba, yule Mohamed Hussein Tshabalala yuko benchi! Hapo kati, namba nne unamkuta Mganda, Juuko Murshid, tano sasa yuko kiraka Erasto Nyoni hawa jamaa wanakaba na kukontroo hadi raha. Kwenye kiungo namba sita utamkuta, Jonas Mkude ambaye Kocha Msaidizi, Masoud Djuma ameshamtangaza kama Mchezaji Bora wa Tanzania kwenye nafasi hiyo.

 

Hapo saba sasa utakutana na Shiza Kichuya, yeye muda wote anazunguka uwanja mzima na hana nafasi maalumu kutokana na majukumu aliyopewa ya kuwachezesha washambuliaji, John Bocco na Emmanuel Okwi kwa muda wote kuwa nyuma ya wachezaji hao na lengo ni kuwadondoshea mipira mbele kwa kupiga safi ndefu.

Njoo kwenye namba nane unakutana na Mghana, James Kotei wengi humuita mgumu kwa maana ya kuwa fiti kutokana na uwezo wake wa kugongana na mchezaji yeyote tofauti na kuchezesha timu, pia ana uwezo mkubwa wa kukaba na mara nyingi hucheza kwa kubadilishana na Mkude wakiwa uwanjani wenyewe wakati mwingine hawaeleweki yupi namba sita, nane. Lakini hapiti mtu.

 

Huku sasa kwenye safu ya ushambuliaji, ndiyo usijaribu kugusa. Gendamarie unaambiwa kocha wao anamjua Laudit Mavugo tu ambaye benchi linamhusu. Fowadi ya Simba ni hatari, namba tisa anasimama John Bocco binadamu anayesifika kwa magoli ya miguu na vichwa, hajawahi kumuogopa beki ukimkwatua ndiyo kwanza anazidi kuja. Namba kumi hapa sasa ndiyo habari ya mjini, Emmanuel Okwi.

 

Yanga walianza kumuita Mhenga lakini baadaye wakalifuta hilo jina wenyewe. Anaongoza katika ufungaji kwenye ligi na mabao yake 13, huyu jamaa Gendamarie hawajawahi kumuona kwa sura lakini baada ya mechi ya leo watamuota. Hapa namba kumi na moja leo atasimama fundi mwenyewe, wa kuitwa, Said Ndemla. Achana naye kwa udambwidambwi juzi tu alipewa zawadi ya gari aina ya Passo na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe kutokana na mavitu yake uwanjani. Sasa ukitaka kuona ufundi wake ndiyo leo sasa, haya ndiyo mashindano yake.

 

Msikie Kocha Kocha Mkuu wa Simba, Pierre Lechantre raia wa Ufaransa, amesema: “Nawafahamu vizuri wapinzani wetu kwa sababu nimeona wakicheza na inafahamika wazi kwamba nchi ya Djibouti hakuna timu za ushindani sana, hivyo tumejipanga kushinda na kusonga mbele.” “Kikosi kipo vizuri mpaka sasa, kilichobaki ni kusubiri muda ufike tucheze mchezo huo na kupata matokeo.Ni lazima nyumbani tucheze soka la kushambulia sana huku tukiwa makini katika kujilinda, mfumo tutakaoutumia ni wa mabeki wanne.

 

Tukienda kurudiana nao tutaweka walinzi kama watano,” alisema. Okwi naye amesema: “Tumejiandaa vizuri na ukiangalia kikosi chetu cha msimu huu kipo vizuri kina wachezaji wengi wazoefu, hivyo tunawaomba mashabiki waje kutusapoti.” Kwa upande wa meneja wa timu hiyo, Richard Robert, amemaliza kwa kusema: “Kwa Simba hii unakaaje nyumbani, mashabiki waje tu uwanjani kushuhudia burudani.”

Loading...

Toa comment