The House of Favourite Newspapers

Simba SC Wampambania Chikwende CAF

0

MABOSI wa Simba wameanza taratibu za kumuombea kibali kiungo wao mshambuliaji Mzimbabwe Perfect Chikwende katika Shirikisho la Soka Afrika (Caf) ili nyota huyo acheze Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Hiyo ni baada ya timu hiyo kukamilisha taratibu za usajili wa nyota huyo katika usajili wa dirisha dogo lililofungwa Januari 15, mwaka huu.Simba imemsajili mshambuliaji huyo kwa ajili ya kuiimarisha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo inayoongozwa na John Bocco, Meddie Kagere na Chris Mugalu.

 

Kwa mujibu wa Crescentius Magori ambaye ni Mshauri Binafsi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, viongozi wa timu hiyo wamejipanga vema kuhakikisha mshambuliaji huyo anapata kibali kutoka Caf ili wamtumie katika michuano hiyo mikubwa Afrika.

Magori alisema kuwa tayari wamekamilisha taratibu zote za kumuombea mshambuliaji huyo kibali Caf baada ya kufuata taratibu ambazo zinahitajika.

 

“Kama uongozi tuna malengo makubwa katika msimu huu na kikubwa ni kuhakikisha tunapambana ili tufike katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mwaka huu hivyo ni lazima tukiboreshe kikosi chetu.“Hivyo katika kukiboresha kikosi chetu tumemsajili Chikwende ambaye yeye tupo katika hatua za mwisho za kupata kibali chake kutoka Caf ili acheze michuano hiyo.

 

“Na mashabiki waondoe hofu katika kumtumia Chikwende katika michuano hii mikubwa Afrika, kwani kanuni mama ya Caf, inasema mchezaji mmoja haruhusiwi kucheza au kuhama zaidi ya timu mbili katika msimu mmoja.

 

“Kutokana na kanuni hiyo tunaweza kumtumia Chikwende kwani amehama klabu moja tu FC Platinum kuja Simba, tutachofanya ni kumuombea kibali cha kucheza Caf, kama watatupatia sawa lakini ikishindikana watatueleza kwa sababu gani hivyo tusubiri huko mbele tuone,” alisema Magori.

Stori: Wilbert Mollandi, Dar es Salaam

Leave A Reply