The House of Favourite Newspapers

Simba SC Watajiwa Bei ya Beki wa Kimataifa

0

UNAAMBIWA bila shilingi milioni 958 za Kitanzania, Simba haiwezi kumpata beki wa kimataifa wa Burundi anayekipiga nchini Afrika Kusini katika Klabu ya Chipa United, Frederic Nsabiyumva.

 

 

Simba imekuwa ikimfuatilia mchezaji huyo kuanzia dirisha lililopita la usajili lakini iligonga mwamba kutokana na thamani yake. Uongozi wa Simba baada ya kupewa ruhusa ya kuongeza wachezaji 10 kwa ajili ya michuano ya kimataifa msimu huu, ina mpango wa kuboresha safu yake ya ulinzi ambayo imekuwa ikiruhusu mabao katika michezo ya ligi kuu jambo ambalo limewafanya kumrudia beki huyo.

 

 

Beki huyo mwenye umri wa miaka 25, anakumbukwa kwa kumkaba vizuri mshambuliaji Mbwana Samatta katika mchezo wa kirafi ki uliofanyika Uwanja wa Mkapa kati ya Tanzania na Burundi na Burundi kuibuka na ushindi wa bao 1-0, Oktoba 11, mwaka huu.

 

 

Kuhusiana na thamani yake, wakala wa wachezaji katika Ligi ya Afrika Kusini anayejulikana kwa jina la Herve Tra Bi, aliliambia Spoti Xtra kuwa ili Simba waweze kumpata beki huyo, lazima walipe si chini ya euro 350,000 ambazo kwa Tanzania ni zaidi ya shilingi milioni 958.

 

 

“Simba wanatakiwa watoe si chini ya euro 350,000, hiyo inatokana na thamani aliyonayo mchezaji huyo na ubora wake bila kusahau umri na ligi anayocheza. Hivyo kama Simba watakuwa tayari kuilipia hiyo nadhani watampata.

 

 

“Ukiangalia Chipa United walimnunua kwa euro 225,000 (zaidi ya Sh milioni 616 za Kitanzania) kutoka Jomo Cosmos, hivyo lazima wamuuze kwa faida,” alisema wakala huyo. Simba licha ya kumhitaji beki huyo, pia wanamhitaji beki wa Biashara United, Abdulmajid Mangalo.

MARCO MZUMBE, Dar es Salaam

 

Leave A Reply