Simba SC ya MO Dewji balaa!

UONGOZI wa Simba chini ya muwekezaji Mohammed Dewji ‘Mo’ ni mafi a kwelikweli. Yaani wakati wapinzani wao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wanajipanga wao wameshaanza harakati za mapambano.

Simba imeshafanya mambo mengi ya msingi ambayo benchi la ufundi linahitaji kuelekea mechi ya kwanza dhidi JS Saoura ya Algeria kwenye Uwanja wa Taifa, Januari 12.

 

Siyo mechi hiyo tu, tayari benchi la ufundi lina mikanda ya video za sasa na maelezo ya timu zote tatu pinzani zinazocheza na Simba ambazo AS Vita ya DR Congo, Saoura ya Algeria na Al Ahly ya Misri.

Akizungumza na Spoti Xtra linalotoka kila Alhamisi na Jumapili, Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Swedy Mkwabi alisema; “Tumetafuta kila kitu kinachohusiana na wapinzani wetu kama mikanda na video za mechi zao tayari zipo mikononi mwetu. “Lengo ni kocha pamoja na wachezaji waanze kufanyia kazi mara moja kutokana na aina ya mashindano yenyewe yanahitaji umakini mkubwa.

“Na hiyo mikanda ambayo tumeipata na kumpatia mwalimu ni timu zote ambazo tumepangwa nazo katika Kundi D na tulitafuta mapema kumrahisishia kazi kocha wetu kuelekea mashindano hayo. “Lakini kama timu malengo yetu ni kufanya vyema katika Ligi ya Mabingwa, kwa sasa tuna majukumu ya mapinduzi lakini maandalizi yanaendelea.”

Kuhusiana na marekebisho kwenye benchi la ufundi Mkwabi ambaye ni mjasiriamali mkubwa mkoani Tanga, alisema; “Mpango wa kusajili mchezaji mwingine upo kwa ajili ya michuano hii, lakini itategemea na matakwa ya kocha, tutakaa naye kujua ni mchezaji wa aina gani ambaye anamuhitaji.

 

“Kwa upande wa kocha msaidizi tutamsikiliza kocha kuona anahitaji kocha wa aina gani ambaye ataona anamfaa na sisi tutabakia kwa ajili ya utekelezaji.”

MCHECHETO Kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii, Saoura wameonyesha kushtushwa na umati wa mashabiki waliohudhuria kwenye mechi ya kufuzu makundi baina ya Simba na Nkana uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar kwani ni jambo geni kwao kwa vile bado wachanga kisoka.

Si hiyo tu, wamekuwa wakifuatilia hatua kwa hatua mechi za Simba kwenye Ligi Kuu Bara.
KOCHA ADHARAU Kocha wa JS Saoura, Nabil Neghiz (pichani) amesema watakuwa na kazi ngumu kwenye kundi lao lakini Simba na AS Vita ni wepesi. Nabil ambaye ni kocha wa Mtanzania, Thomas Ulimwengu, alisema Al Ahly ndiyo timu pekee inayompa wasiwasi kwenye kundi hilo.

 

“Kundi letu ni gumu,Ahly ni klabu kubwa ya karne itakuwa ni mechi ngumu sana. Nadhani Simba na Vita siyo timu ngumu kwetu, tunahitaji kuweka mipango sawa tu. “Tuna maelezo kiasi fulani kuhusiana na Simba, lakini tutapambana nao kimkakati.”

MARTHA MBOMA NA KHADIJA MNGWAI

Loading...

Toa comment