The House of Favourite Newspapers

Simba Sc Yaanika Mbinu Walioitumia Kuiua AS Vita

0

 

OFISA Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, amesema ushindi ambao timu yao iliupata katika mechi ya kwanza ya Kundi A ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), ulichangiwa na mbinu ‘mbadala‘.

 

 

Barbara aliliambia gazeti hili mechi hiyo haikuwa rahisi na kuitaja moja ya mbinu iliyowapa ushindi ni ‘kuwapeleleza‘ vyema wapinzani wao.

 

 

Kiongozi huyo alisema kwa sasa wao kama Simba wamewekeza sana kwenye ‘kuwasoma na kupeleleza’ wapinzani wao na ndiyo kwa kiasi kikubwa kimewafanya wapate ushindi wa bao 1-0 na kukaa kileleni kwenye kundi lao.

 

 

“Mpaka kuna mwenyekiti mmoja wa zamani wa klabu yetu amenipigia simu na kunipongeza akisema Barbara hongereni, kupata ushindi Congo si jambo rahisi,” alisema kiongozi huyo.

 

 

 

Alisema mazingira yalikuwa magumu na haikuwa kazi rahisi kupata ushindi kama si wao viongozi, benchi la ufundi na wachezaji kupambana kufanya kazi iliyotakiwa kufanyika katika mechi hiyo.

 

 

“Haikuwa rahisi, unajua hivi sasa nimewekeza sana kwenye mbinu ya kuwasoma na kuwapeleleza wapinzani. Kujua nguvu yao iko wapi na udhaifu wao ulipo, ili kujua unapambana nayo vipi kuziba mianya na nguvu yao na kutumia udhaifu wao ili kupata ushindi,” alisema Barbara.

 

 

Hivi karibuni, Simba ilimwongeza Mzimbabwe Culvin Mavhunga kwenye benchi la ufundi ambaye ni mchambuzi wa masuala ya soka, aliyekuwa akiifanyia kazi hiyo katika kikosi cha FC Patinum na Chama cha Soka nchini Zimbabwe.

 

 

Mavhunga ni mtaalamu wa kujua na kuchambua viwango vya wachezaji wa timu pinzani, hivyo Klabu ya Simba baada ya mechi kati ya timu hiyo dhidi ya FC Patinum, ilimchukua kwa kazi hiyo tu ya kupeleleza na kujua mfumo, mbinu, nguvu na udhaifu wa timu pinzani.

 

 

Leave A Reply