Simba SC Yahamishia Hasira Zote kwa Biashara United

UONGOZI wa Simba umesema kuwa kwa sasa umeweka nguvu zake zote katika mchezo wao wa kwanza wa ligi kuu dhidi ya Biashara United katika mchezo utakaofanyika leo Jumanne katika Uwanja wa Karume mkoani Mara.

 

Simba Jumamosi ilipoteza mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii kwa kufungwa bao 1-0 na Yanga katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Mkapa uliopo Dar es Salaam.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, CEO wa Simba, Barbara Gonzalez alisema kuwa kwa sasa wamewekeza nguvu zao zote katika mchezo wao wa ligi kuu dhidi ya Biashara United utakofanyika ugenini huku akiweka wazi kusahau kilichotokea katika mchezo uliopita ambao walipoteza dhidi ya Yanga.

 

“Tunamshukuru Mungu vijana wetu walipambana lakini haikuwa fungu letu kwa wanasimba kuwa mabingwa na kwa sasa tumesahau yote ambayo yametokea kwani ni sehemu ya matokeo ya mpira wa miguu na kwa sasa tunaangalia mchezo wetu wa ufunguzi dhidi ya Biashara.

 

“Biashara wanapokuwa nyumbani kwao wamekuwa na matokeo mazuri hivyo ni lazima tukapambane ili kuhakikisha tunarudi na matokeo mazuri ambayo yatatufanya tusahau kupoteza katika mchezo wetu dhidi ya Yanga,” alisema kiongozi huyo.

MARCO MZUMBE, Darb es Salaam


Toa comment