The House of Favourite Newspapers

Simba vs Yanga… Mtanuna Tena Mbonaaa

0

LEO Jumamosi kabla hata watu hawajapata msosi wa usiku tayari ule ubishi wa nani atabeba ubingwa wa Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga ambao unaendelea mtaani utakuwa ushatatuliwa.

 

Ubishi huo umezua maneno mengi ambapo baadhi ya mashabiki wakiwaambia wenzao kwamba watanuna tena baada ya kuwafunga.

 

Kuhakikisha timu hizo zinapata ushindi leo, mabosi wa timu hizo wameweka fedha za kutosha kwa wachezaji wa vikosi hivyo kwa ajili ya kufanikisha wanapata ushindi mbele ya watani zao.

 

Mabosi wa Yanga kwa upande wao waliweka mezani kwa mastaa wao bonasi ya nusu bilioni kama wakifanikiwa kuwafunga watani wao wa jadi Simba huku wenzao wa Simba nao wakijibu kwa kuweka kiwango hicho mezani.

 

Mchezo huo wa Ngao ya Jamii unatarajiwa kupigwa leo saa kumi na moja jioni kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

 

Mmoja wa mabosi wa Yanga, ameliambia Championi Jumamosi kuwa bonasi hiyo waliahidi juzi katika kikao cha pamoja cha kamati ya mashindano ya timu hiyo, wachezaji na benchi la ufundi.

 

Bosi huyo alisema kuwa wameahidi kuwapa bonasi hiyo kwa ajili kuongeza morali na hali ya kujituma kwa wachezaji wao ili kuhakikisha wanapata ushindi kwa ajili ya kurejesha furaha ya mashabiki wao baada ya kutolewa katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

“Mchezo huu una umuhimu mkubwa kwetu Yanga, kwanza ni kurejesha furaha kwa mashabiki wetu ambao walijitoa kwa wingi katika tamasha letu la Wiki ya Mwananchi. Hivyo hatutaki kuona wakipotea uwanjani wakati timu ikiwa inacheza, hivyo ili waendelee kujitokeza ni lazima tupate matokeo mazuri kwa kuanzia mchezo huu wa Ngao ya Jamii.

 

“Kama uongozi tulifanya kikao cha binafsi kwa ajili ya kuweka mikakati ya ushindi, pia tulikutana na wachezaji, benchi la ufundi kwa ajili ya kutoa hamasa ikiwemo kuahidi bonasi hiyo ya fedha,” alisema bosi huyo.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa Yanga, Rogers Gumbo alizungumzia hilo kwa kusema kuwa: “Leo (jana) asubuhi tuliendelea na kikao cha maandalizi ya mchezo wa Ngao ya Jamii. Kikubwa ni kuweka mikakati ya ushindi, tunafahamu umuhimu mkubwa wa mchezo huu na kuhusu bonasi ya wachezaji hilo lipo kwa muda mrefu tumekuwa tukiwapa pale wanapopata ushindi na katika mchezo huu ipo bonasi yao ambayo ni siri kati ya wachezaji na viongozi.”

 

Kwa upande wa Simba kwa mujibu ambazo Championi Jumamosi lilipata kabla ya kwenda mtamboni ni kuwa waliwekewa kiasi cha milioni 500 ikiwa ni ahadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya timu hiyo, Mohammed Dewji.

 

“Mo alikuwa tayari kutoa ahadi ya kiwango cha bonasi kwa wachezaji, lakini ameshindwa kufanya hivyo kwa hofu ya wachezaji kucheza kwa presha. Licha ya kuficha lakini ameahidi kutoa mara mbili ya bonasi ambayo wamekuwa wakipata katika msimu uliopita na kiwango kinachokadiliwa ni Sh 500Mil.

 

“Katika kikao amesisitiza ushindi kwani huo utakuwa mwanzo mzuri kwao katika kuelekea msimu ujao ambao ni mgumu kwao baada ya kubeba Ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Kaimu Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga kuzungumzia hilo alisema kuwa “Ni kweli Mo alikwenda kuitembelea na timu mazoezini na kuzungumza kidogo na wachezaji na kikubwa ni kuwaongezea morali.

 

“Kuhusu bonasi hiyo ni siri ya timu, tunafanya hivyo kwa hofu ya kuwagombanisha wachezaji na familia zao baada ya ushindi.”

WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA, Dar es Salaam

Leave A Reply