The House of Favourite Newspapers

Simba: Wasauzi Watakula za Kutosha

0

IKIWA na kibarua kizito leo katika Uwanja wa FNB ‘Soccer City’ uliopo Johannesburg nchini Afrika Kusini, kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba tayari wamefanikiwa kukwepa fitna za Kaizer ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi leo.

 

Simba leo inatarajiwa kucheza na miamba hiyo ya Afrika Kusini katika mchezo unaotarajiwa kupigwa saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki kwenye Uwanja wa FNB huku wakitarajia kurudiana Mei 22, katika Uwanja wa Mkapa uliopo Dar es Salaam.

 

Taarifa ambazo Championi Jumamosi imezinasa kutoka kwa vyanzo vyetu vya kuaminika vilivyo nchini Afrika Kusini, ni kuwa, katika kuhakikisha kikosi cha Simba kinaondoka na ushindi, tayari kimenasa faili zima la Kaizer Chiefs, hiyo ni baada ya kufanikiwa kuwatuma maofisa wake kwenda kushuhudia mchezo wa mwisho ambao Kaizer walicheza dhidi ya Moroka Swallows Jumatano iliyopita, ulioisha kwa sare ya bao 1-1, na pia walifanikiwa kuingia katika mazoezi ya timu hiyo mara mbili mfululizo.

 

“Kila kitu kinakwenda vizuri, katika kuhakikisha kuwa timu inafanya vizuri tulifanikiwa kupitisha baadhi ya maofisa wetu kwenye mchezo wa mwisho ambao Kaizer Chiefs walifanikiwa kucheza dhidi ya Swallows ambapo walitoka sare ya bao 1-1.

 

“Pia katika mazoezi ya mwisho kufanywa na Kaizer, kuna wataalamu wetu tuliwaagiza na walifanikiwa kupenya kisha kuangalia kila kitu kinachoendelea, kwa hiyo tumepata baadhi ya mbinu zao ili kufahamu namna gani tutawakabili,” kilisema chanzo hicho.

 

Pia mchezo wa leo hautakuwa na mashabiki kutokana na kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Corona.

 

KOCHA GOMEZ AZUIWA

Aidha siku ya mechi ya Kaizer na Swallows chanzo kimesema Kocha wa Simba, Didier Gomes alizuiwa kwenda kuangalia mchezo huo.

 

“Gomes alihitaji kwenda kuwatazama Kaizer Chiefs wakicheza lakini yeye alizuiwa kwa kuwa wapinzani wetu walimtambua na kumzuia asiingie uwanjani, lakini baadhi ya maofisa wengine walifanikiwa kupenya na kushuhudia mchezo huo.”

 

MZIMBABWE AHUSIKA

“Culvin Mavhunga Mzimbabwe wa Simba ambaye ni mtaalamu wa kuchambua viwango vya timu ya Simba pamoja na wapinzani ni mmoja wa maofisa wa Simba ambao waliushuhudia mchezo huo, hivyo tayari atakuwa ameshapeleka taarifa kwenda kwa kocha mkuu, Didier Gomes na huyo ndiye kazi yake, aliajiriwa kwa ajili ya kufanya kazi hizo.

 

SIMBA WAFUNGUKA

Akizungumzia maandalizi yao, Mratibu wa Klabu ya Simba, Abbas Ally, alisema: “Tumefanikiwa kuwaona Kaizer Chiefs katika mchezo wao uliopita dhidi ya Moroka Swallows na kufanikiwa kuangalia wapi wana upungufu bila kusahau ubora wao ili kujua namna gani tunaweza kuwakabili.

 

“Tunafahamu kuwa Kaizer ni timu nzuri na yenye historia kubwa ndani ya Bara la Afrika lakini tumekuja hapa kupambana na kuhakikisha tunafikia malengo ya kusonga mbele.”

 

HUYU HAPA GOMES

“Maandalizi tuliyoyafanya yanatosha kabisa kutupa ushindi mbele ya Kaizer, wana timu nzuri na wachezaji bora lakini mara zote dakika 90 ndizo zinatoa majibu. Nasi tunaamini tutapata ushindi.”

 

BARBARA NAYE AFUNGUKA

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba (CEO), Barbara Gonzalez alisema: “Morali ya kikosi chetu kuelekea mchezo dhidi ya Kaizer ni kubwa, licha ya kuwa na changamoto kidogo ya hali ya hewa lakini tumejipanga vizuri kupata matokeo chanya.

 

“Sisi kama viongozi tayari tumeshamaliza mipango yetu nje ya uwanja ikiwemo kuwachunguza wachezaji gani hatari kwao. Lakini pia kuwapa motisha ya kuwa kuna bonasi kubwa watapata kama watashinda mchezo huo.

“Tuliwaambia kuwa huu ni mchezo muhimu pengine kuliko mechi nyingine tulizocheza kwa sababu inatupeleka kwenye lengo letu la kutinga nusu fainali.”

 

WALICHOKISEMA KAIZER CHIEFS

Kupitia mitandao yao ya kijamii, timu ya Kaizer iliandika: “Kwa sasa mawazo yetu yote ni katika mchezo wetu ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Simba, na tuko tayari kwa mchezo huo, tunajua Simba ni wapinzani wagumu kwetu lakini tuna matarajio makubwa ya kufanya vizuri, tunawaomba mashabiki wetu watusapoti.”

 

KIKOSI CHA SIMBA KINACHOTARAJIWA KUANZA

1.Aishi Manula 2. Shomari Kapombe, 3. Mohammed Hussein, 4. Joash Onyango, 5. Pascal Wawa, 6. Thadeo Lwanga, 7. Clatous Chama, 8. Jonas Mkude, 9. Chris Mugalu, 10. Larry Bwalya, 11. Luis Miquissone.

Leave A Reply