The House of Favourite Newspapers

Simba Watamba Tunawapiga Nje, Ndani Kaizer Chiefs

0

SIMBA inatarajiwa kushuka uwanjani kesho Jumamosi katika mchezo ambao inawezekana ukawa ni mwendelezo wa timu hiyo kuandika historia ya kipekee kama watafanikiwa kusonga mbele na hatimaye kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Matumaini ya Simba kufanya vizuri msimu huu, yanakuja kwa kuwa kumekuwa na imani hiyo kutokana na mwendelezo wao mzuri katika michuano hiyo msimu huu tofauti na ilivyokuwa miaka mingine ya nyuma.

Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, amefunguka kuwa, ana uhakika timu yake itapata matokeo dhidi ya Kaizer Chiefs kwenye mechi zote mbili.

Barbara amesema alikaa na kocha, wachezaji pamoja na benchi la ufundi la timu yake, akabaini kuwa kila mtu morali yake ipo juu, hivyo kuna kila sababu ya wao kupata ushindi kwenye mechi hizo.

 

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo kwa upande wa uongozi, Barbara alisema wameshamaliza kila kitu na wamewaambia wachezaji bonasi watakayopata kwa kushinda mchezo huo, hivyo hana wasiwasi kwa kuwa anajua wachezaji wake hawawezi kumuangusha.

 

“Naona kabisa tukishinda mechi zote mbili kwa uwezo wa Mungu, tutawafunga Kaizer hapa Afrika Kusini na tutakwenda kuwafunga pia kwenye uwanja wetu wa nyumbani pale kwa Mkapa.

“Sisi kama viongozi tumeshacheza party yetu na wachezaji wanajua bonasi gani watapata kama watashinda hapa na nini watakivuna wakishinda Dar.

 

Huu ni mchezo muhimu kuliko michezo mingine yote waliyocheza msimu huu,” alisema Barbara.Simba wanatarajia kushuka kwenye Uwanja wa Soccer City kutupa karata yao ya kwanza kwenye Hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs.

 

KAIZER WAVURUGANA, MASHABIKI WAINGILIA

Wakati huohuo, mshambuliaji na nahodha wa Kaizer, Bernard Parker ameingia matatizoni muda mfupi kabla ya mchezo wa Simba kutokana na kuonyesha utovu wa nidhamu katika mechi dhidi ya Swallows FC, juzi Jumatano.

Kamera zilimnasa staa huyo akimtolea maneno makali mshambuliaji mwenzake, Samir Nurkovic wakati wa mcheo huo wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, tukio ambalo limewakera baadhi ya mashabiki wa timu yake na kumjia juu nahodha wao.

 

Kauli za nahodha huyo zilikuwa kali hali ambayo imefanya kuwe na maneno mengi kutoka kwa mashabiki wa Kaizer ambao wanajulikana kwa kutoendekeza nidhamu mbovu kwa memba wa klabu yao iwe ndani au nje ya uwanja.Meneja wa Kaizer, Vina Maphosa amesema hajapata malalamiko rasmi lakini atazungumza na uongozi kisha watatoa tamko.

 

Tukio hilo linaweza kuwatoa mchezoni wachezaji kama presha itaendelea kuwa kubwa kwa kuwa wanakutana na Simba, kesho huku wakiwa hwana matokeo mazuri katika mechi za ligi kuu.

STORI NA JOHN JOSEPH NA ISSA LIPONDA | CHAMPIONI IJUMAA

Leave A Reply