The House of Favourite Newspapers

Simba Watangaza Kiama cha Al Ahly ya Misri

0

KOCHA Mkuu wa Simba, Mfaransa, Didier Gomes, amesema kuwa ushindi walioupata dhidi ya AS Vita umewajengea hali ya kujiamini wachezaji wake na kupata matokeo mazuri katika mchezo ujao wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Simba katika mchezo ujao wa Kundi A, inatarajiwa kuvaana na Al Ahly ya Misri ambayo mchezo wao wa kwanza ilifanikiwa kuwafunga Al Merrikh mabao 3-0.

 

Mchezo huo dhidi ya Al Ahly unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa, umepangwa kupigwa Februari 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.Ikumbukwe timu hizo zote zina pointi tatu huku Ahly wakiwa juu katika msimamo wa Kundi A kwa tofauti ya mabao ya kufunga.

Akizungumza na Championi Jumamosi,Gomes alisema kuwa katika kuelekea mchezo huo wapo tayari kupambana kwa kutoa kile walichonacho ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ya ushindi.

 

Gomes alisema kuwa anaamini vijana wake wameongeza hali ya kujiamini baada ya kuwafunga AS Vita nyumbani kwao, kwani siyo kitu kidogo baada ya misimu mitatu mfululizo timu hiyo kushindwa kupata matokeo ugenini.

 

Aliongeza kuwa hivi sasa anaendelea kukifanyia maboresho kikosi chao ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika michezo inayofuatia ya michuano hiyo ya kimataifa sambamba na Ligi Kuu Bara.“Tupo tayari kupambana na tupo tayari kutoa kila tulichonacho.

Al Ahly ni timu nzuri ambayo nimeiona katika mchezo wao uliopita dhidi ya Merrikh.“Inacheza mfumo mzuri lakini tupo kwenye hali nzuri ya kujiamini na hasa baada ya ushindi wa DR Congo.

 

Tunahitaji pointi tatu ili tukae katika nafasi nzuri katika msimamo wa Kundi A. “Licha ya vijana wangu kujiamini lakini ninaendelea kukifanyia maboresho kikosi katika sehemu zenye upungufu kwa ajili ya kupata matokeo mazuri kwani bado tuna kibarua kigumu katika kundi hili gumu,” alisema Gomes.

 

WACHEZAJI WAGOMEA MAPUMZIKO

Mastaa wa Simba ilikuwa wapate mapumziko baada ya kutoka Mara jana walikokuwa wakicheza na Biashara United na kushinda bao 1-0, wamegomea na kuitaka kuendelea na kambi kwa ajili ya mechi dhidi ya Al Ahly. Wachezaji hao wamegomea mapumziko hayo kwa kuwa wanajua kuwa mchezo ujao ni mgumu hivyo wameunga moja kwa moja kambini kwa ajili ya maandalizi kabambe.

 

YATANGAZA KAULI MBIU MPYA

Aidha akizungumza na Waandishi wa Habari, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Simba, Haji Manara alitangaza kauli mbiu mpya ambayo wataitumia kuelekea kwenye mchezo huo dhidi ya Al Ahly ambayo ni Total War, Point of No Return.

 

“Katika mchezo wetu na FC Platinum ya Zimbabwe tulitumia kauli mbiu ya War in Dar lakini kuelekea katika mechi kubwa kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati kwa sababu Simba ndiyo timu pekee inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua ya makundi tutatumia kauli mbiu ya Total War, Point of No Return yaani vita kamili, hakuna kurudi nyuma maana malengo yetu ni kushinda sasa hatuwezi kukubali kurudi nyuma.

 

”BUKU TATU KUWAONA AL AHLY KWA MKAPA

Katika upande wa viingilio, Manara alisema kuwa wamepanga kiingilio cha Sh 3,000 kwa watu wa mzunguko, VIP B itakuwa ni Sh 15,000 na Sh 30,000 kwa VIP A lakini viingilio hivyo vitabadilika siku ya Jumatatu saa sita usiku na kuwa Sh 5,000 kwa mzunguko, Sh 20,000 kwa VIP B wakati VIP A ikiwa ni Sh 40,000.

 

AL AHLY WATUA

Wakati huohuo Manara amesema kuwa wapinzani wao walitarajiwa kutua nchini usiku wa kuamkia leo tayari kwa mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

 

TIMU KIGOGO YAIPOKEA AL AHLY

Katika hatua nyingine Manara alisema kuwa: “Tumepata taarifa za moja ya timu kubwa hapa nchini inafanya uratibu wa mapokezi ya wapinzani wetu Al Ahly kwa kuwatafutia uwanja wa kufanyia mazoezi.“Kwetu sisi tunachukulia kawaida na hatuhofii juu ya hicho wanachokifanya na badala yake sisi tunajikita kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wetu.”

Leave A Reply