The House of Favourite Newspapers

Simba Yaahidi Kupindua Uwanja wa Mkapa

0

LICHA ya Simba jana kufungwa bao 1-0 dhidi ya FC Platinum, lakini benchi la ufundi na nyota wa kikosi hicho wameahidi kupindua matokeo jijini Dar es Salaam.

 

Jana Jumatano, Simba ikiwa Harare nchini Zimbabwe, ilipoteza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa bao 1-0 lililofungwa dakika ya 17 na Perfect Chikwende.

 

Mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimbabwe, ulikuwa na kosakosa nyingi kutoka kila upande.

Bao la FC Platinum lilitokana na Chikwende kuwazidi mbio walinzi wa Simba akiwemo Pascal Wawa.Kabla ya mchezo huo wa jana, Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alisema ataikosa huduma ya mshambuliaji wake, John Bocco na kipa Aishi Manula, lakini Manula alicheza, huku Bocco akikosekana.

 

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo, zinasema kwamba, muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Sven alizungumza na wachezaji wake katika kuwatuliza, kisha kwa pamoja kukubaliana kuja kumaliza kazi nyumbani.

 

Simba na FC Platinum, zinatarajiwa kurudiana Januari 6, mwakani katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar ambapo mshindi wa jumla anakwenda hatua ya makundi, atakayeondolewa anaangukia hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kufungwa kwa Simba ugenini jana, inakumbusha ilivyotokea msimu wa 2018/19 katika hatua kama hii ambapo walifungwa ugenini 2-1 na Nkana FC ya Zambia, kisha nyumbani ikashinda 3-1 na kutinga makundi, hivyo matokeo hayo yanawapa jeuri ya kupindua meza.

 

NAMUNGO YAFANYA KWELI

Wawakilishi wengine wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, Namungo, jana waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Al Hilal Obeid ya Sudan katika Kombe la Shirikisho Afrika, mchezo uliochezwa jana Uwanja wa Azam Complex, Dar.

Mabao ya Namungo yalifungwa na Sixtus Sabilo dakika ya 13 na Stephen Sey dakika ya 30.Timu hizo zinatarajiwa kurudiana kati ya Januari 5-6, mwakani.

Leave A Reply