The House of Favourite Newspapers

Simba Yaandika Historia Bongo

0

RASMI sasa Klabu ya Simba imeandika historia yake mpya ambapo, Jumatatu hii timu yake ya soka itaanza kutumia viwanja vyake viwili vilivyopo Bunju jijini Dar baada ya ujenzi wa awamu ya kwanza kukamilika.

 

Viwanja hivyo vilivyopewa jina la Bunju Complex, vimetumia siku 120 hadi kukamilika kwake na sasa klabu hiyo itapata fursa ya kuwa na sehemu yao ya kufanyia mazoezi.

Hatua hiyo inakuja ikiwa leo, jopo la wanachama, mashabiki wa klabu hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na Mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ kufungua rasmi viwanja hivyo ili vianze kutumika.

 

Simba wameingia kwenye historia ya kuwa miongoni mwa klabu zinazomiliki viwanja vyake, wakijenga viwanja viwili tofauti katika eneo moja, kimoja cha nyasi za kawaida na kingine cha nyasi bandia.

Championi Jumamosi lilitembelea eneo hilo jana asubuhi na kushuhudia mabadiliko makubwa katika ujenzi huo, huku kila kitu kikionekana kukamilika na jopo la wafanyakazi wa mradi huo wakiwemo akina mama wakifanya usafi wa mwisho kuzunguka viwanja vyote tayari kwa sherehe za ufunguzi.

 

Edward Shirima ambaye ni msimamizi na mkandarasi wa mradi huo amezungumza na Championi Jumamosi na kusema: “Tupo katika hatua za mwisho ili kukabidhi mradi huu kama ambavyo mnaona, kubwa zaidi kwa siku ya leo ni kufanya usafi ikiwa ni pamoja na kuchora mistari kwenye huu uwanja wa nyasi asilia.

“Hata hivyo mpaka kufika hapa napenda kuupongeza uongozi wa Simba kwani hakuna kitu chochote kinachohusiana na fedha ambacho kilitukwamisha. “Kila kitu tulikuwa tunakipata kwa wakati bila ya tatizo lolote lakini kwa upande wa maalipo ya ujenzi huo tumeridhika  kwa asilimia miamoja,” alisema Shirima.

 

Ndani ya uwanja huo kuna vyoo vya mashimo matatu na vile vya haja ndogo vya kisasa viko vitatu, kuna mabafu matatu sehemu ya kubadilishia nguo ni moja na tayari umeme na maji tayari vipo. Imeandikwa na Sweetbert Lukonge, Issa Liponda na Abdulghafal Ally

Leave A Reply