The House of Favourite Newspapers

ads

Simba Yaifanyia Balaa Zito Horoya AC, Yatinga Robo Fainali Ligi ya Mabingwa

0

SIMBA wanawaambia semeni tena juu ya timu yao kwamba haifungi mabao mengi, hiyo ni baada ya jana kufanya balaa zito mbele ya Horoya AC,

Katika mchezo huo wa Kundi C kunako Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 7-0 na kukata tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali ikisaliwa na mchezo mmoja ugenini dhidi ya Raja Casablanca.

Usifanye mchezo na Mwamba wa Lusaka, Clatous Chama, kwani jana aliwaka sana kunako kikosi cha Simba akifunga mabao matatu ‘hat trick’.

Chama alifunga mabao hayo dakika ya 9 kwa faulo ya moja kwa moja, kisha dakika ya 35 kwa penalti. Bao la tatu, Chama alifunga dakika ya 65.

Hii ni hat trick ya kwanza kwa mchezaji wa Simba katika michuano ya CAF, pia ni ya kwanza kwa Chama kwenye michuano hiyo tangu ajiunge na kikosi hicho.

Mabao mengine ya Simba yalifungwa na Jean Baleke dakika ya 31 na 64, huku Sadio Kanoute akifunga dakika ya 54 na 82.

Simba jana iliingia ikiwa na akili moja tu ya kuibuka na ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu robo fainali ya michuano hiyo, malengo yakatimia.

Kikosi hicho chini ya Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akisaidiwa na Juma Mgunda, kilianza hatua ya makundi kikiwa kinyonge baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za kwanza.

Simba ilianza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Horoya ikiwa ugenini, kabla ya kuchapwa 0-3 nyumbani dhidi ya Raja Casablanca.

Mchezo wa tatu, Simba ikashinda ugenini bao 0-1 dhidi ya Vipers ya Uganda kwa bao la Henock Inonga, kisha nyumbani ikaichapa tena Vipers 1-0, mfungaji akiwa Chama.

Katika mechi nne za kwanza kabla ya jana, Simba ilikuwa imefunga mabao mawili na kuruhusu manne.

Jana ndiyo ilikuwa siku ya Simba kufanya balaa ndani ya Uwanja wa Mkapa na kuziba midomo ya wale wote walioanza kuishushia heshima timu hiyo ambayo kwa takribani misimu mitano nyuma, imecheza hatua ya robo fainali ya CAF mara mbili.

Ushindi wa mabao 7-0 jana dhidi ya Horoya, ni mkubwa zaidi kwa Simba katika michuano ya CAF hatua ya makundi, hakuna kocha aliyewahi kufanya hivyo zaidi ya Robertinho raia wa Brazil.

Simba sasa imefikisha pointi tisa na kuwa nyuma ya Raja Casablanca inayoongoza Kundi C ambazo zote zimefuzu hatua ya robo fainali zikiwa na mchezo mmoja mkononi.

Mchezo wa mwisho wa Kundi C, Simba itakuwa ugenini nchini Morocco kucheza dhidi ya wenyeji wao, Raja Casablanca ukiwa ni wa kukamilisha ratiba tu.

Horoya yenyewe kipigo cha jana, kimewafanya kubaki na alama zao nne katika nafasi ya tatu, huku Vipers ikiburuza mkia.

Vipers na Horoya zikienda kupambana katika mchezo wa mwisho, hata mmojawapo akipata ushindi, hakuna ambaye atawapiku Simba, hivyo shughuli itakuwa imeishia hapo.

Ni furaha kubwa kwa Simba kutokana na ushindi wa jana ambao umewafanya kujihakikishia kitita cha shilingi milioni 35 kutoka kwenye ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye aliahidi kila bao kwa timu za Simba na Yanga hatua ya makundi, atatoa shilingi milioni tano.

Simba ambayo hadi sasa imefunga mabao tisa hatua ya makundi, imekusanya shilingi milioni 45 kutoka kwa Rais Samia.

Leave A Reply