The House of Favourite Newspapers

Simba Yaifuata Al Merrikh Kimafia

0

MSAFARA wa wachezaji 25 wa Simba na viongozi saba, jana Jumatano ulisafiri kuelekea nchini Sudan kimafia tayari kucheza mchezo wa tatu wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh, huku kiungo mshambuliaji Mghana, Bernard Morrison akibakishwa Dar.

 

Simba inayoongoza Kundi A katika michuano hiyo ikiwa na pointi sita, inatarajiwa kuvaana na Al Merrikh keshokutwa Jumamosi.

Timu hiyo jana ilionekana kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam wakiwa na mafuta ya kupikia na maji ya kunywa waliyosafiri nayo ikiwa ni njia mojawapo ya kuepuka hujuma za wenyeji wao.

Akizungumza na Spoti Xtra, Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa Didier Gomes, alisema kuwa maandalizi aliyoyafanya ya kikosi chake yanatosha kupata ushindi katika mchezo huo mgumu wa ugenini.

Gomes alisema kuwa anafahamu upungufu walionao wapinzani wao kutokana na kuwahi kukinoa kikosi hicho kabla ya kujiunga na Simba hivi karibuni.

 

Alisema kuwa katika mazoezi ya mwisho ya juzi Jumanne, ameona vijana wake wakifanya kwa morali kubwa katika kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

 

“Naifahamu vizuri Al Merrikh kutokana na kuwahi kuifundisha, lakini licha ya kuwajua ninaamini mchezo utakuwa mgumu kutokana na wapinzani wetu hao kupoteza michezo miwili iliyopita, hivyo hawatakubali kupoteza tena.“

Hivyo tutaingia katika mchezo kwa nidhamu ya juu ili kuhakikisha tunapata ushindi katika mechi hii kwa lengo kubwa la kuendelea kukaa kileleni katika msimamo wa kundi letu,” alisema Gomes na kuongeza kuwa.“Wachezaji watano niliowaacha akiwepo Morrrison hawana tatizo lolote, nimewaacha kutokana na kutokuwa chaguo langu katika kikosi changu kitakachocheza dhidi ya Merrikh.“

 

Hayo maamuzi sijayachukua mimi pekee, benchi la ufundi ndiyo lililokaa kwa pamoja na kupendekeza wachezaji watakaosafiri kwenda Sudan, hivyo Morrison na wenzake Ndemla (Said), Ame (Ibrahim), Lokosa (Junior) na Chikwende (Perfect) yeye hakusajiliwa kwa ajili ya michuano hii.

”Kwa upande wa uongozi wa timu hiyo, Crensentius Magori ambaye ni Mshauri wa Mjumbe wa Kamati ya Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, alisema kuwa wamejipanga vizuri katika kuelekea mchezo huo na kikubwa ni kuchukua pointi tatu ugenini.

Magori alisema kuwa kama uongozi wanafahamu Merrikh watatumia mbinu na njia zote kuhakikisha wanapata ushindi Simba yaifuata Al Merrikh kimafiakatika mchezo huo, hivyo nao wanauchukulia umuhimu mkubwa mchezo huo kwa lengo la kumaliza makundi wakiwa kileleni.

 

“Merrikh siyo timu nyepesi kama watu wanavyofikiria baada ya kupoteza michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita na Ahly, hivyo tunaamini wataingia uwanjani kivingine kwa lengo la kupata matokeo mazuri baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo na kama wakipoteza na huu watakuwa wametoka katika mashindano.

 

“Tumewaandalia bonasi nzuri wachezaji wetu, kwani huo ndiyo utaratibu tulioupanga katika kila mechi kutokana na ukubwa wa timu tunayokutana nayo, hivyo wanafahamu kabisa wenyewe wakishinda watachukua kiasi gani cha pesa,” alisema Magori aliyekuwa pamoja na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Zakaria Hans Pope ambao wote wamesafiri na timu jana.

 

Naye kipa namba moja wa timu hiyo, Aishi Manula aliyepoteza fahamu katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania na kukimbizwa hospitalini, alisema: “Nimepata nafuu ya majeraha yangu na hivi sasa ninaendelea vizuri.

 

“Kiukweli nilipata majeraha makali sana, kwani hadi ninaanguka chini nilikuwa sijui lolote kutokana na kupoteza fahamu nikiwa juu.“

 

Nashukuru matibabu niliyoyapata mara baada ya kupata majeraha hayo na niwatoe hofu mashabiki wa Simba kwa kuwaambia kuwa nipo fiti kwa ajili ya mchezo dhidi ya Merrikh, licha ya kuyasikia maumivu ya kichwa na tumbo, hivi sasa nipo chini ya uangalizi wa madaktari wa timu.”

”WAANDISHI: WILBERT MOLANDI, MUSA MATEJA NA LEEN ESSAU

Leave A Reply