Simba Yaifuata AS Vita Kijeshi, Yabeba Maji

KIKOSI cha Simba, kinatarajiwa kuondoka leo Jumanne kuelekea nchini DR Congo tayari kwa mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Simba, wanatarajiwa kuondoka wakiwa na kikosi kamili cha kazi akiwemo Jonas Mkude ambaye hivi karibuni alisimamishwa kwa utovu wa nidhamu.

 

Ijumaa ya wiki hii, Simba ikiwa ugenini, inatarajiwa kuvaana na AS Vita katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ambapo timu hizo zimepangwa Kundi A na timu za Al Marreikh na Al Ahly.

 

Mtoa taarifa wetu alidokeza kwa kusema: “Baada ya mchezo dhidi ya Azam FC, kikosi kilipumzika kidogo kisha Jumanne, kinatarajiwa kwenda DR Congo tayari kwa mchezo dhidi ya AS Vita.

“Kikosi ambacho kitaenda ni kamili kile cha uhakika akiwemo Jonas Mkude ambaye kocha amemjumuisha kuongeza nguvu kwenye eneo la kiungo cha ukabaji.“Kutokana na kuhofia michezo michafu ya wapinzani, tutaenda na kila kitu chetu ikiwemo vyakula na maji, tukiwa huko

tutatumia vyakula vyetu, kama tukikosa sehemu nzuri ya kupikia, tutaenda kula ubalozini.“Unajua katika mechi za kimataifa kuna umafia mwingi unafanyika, hivyo hatutaki kuingia kwenye mtego wa kupoteza mechi kizembe.

 

“Ukiachana na hilo, tayari kuna watu wetu wameshatangulizwa huko kwenda kuandaa mazingira ya ushindi ambapo kwa kushirikiana na DC Motema Pembe ya kule DR Congo, tumepata uwanja mzuri ambao tutafanyia mazoezi.

”Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa, Didier Gomes, amesema: “Tunatakiwa kucheza na AS Vita kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza mbele ya Azam FC ambapo tulitakiwa kufunga zaidi ya mabao matatu hadi manne lakini hatukufanya hivyo.

 

“Naamini tukicheza kwa kiwango kile basi mambo yatakuwa mazuri katika mechi hiyo japokuwa kuna vitu vya kurekebisha hasa katika kumalizia nafasi ambazo tunazitengeneza ambazo ni nyingi mno.”

Toa comment