The House of Favourite Newspapers

Simba Yaingilia Usajili Yanga

VITA kubwa ya usajili imehamia kwa beki wa kati wa timu ya taifa, Taifa Stars na klabu ya Coastal Union, Bakari Mwamnyeto anayewaniwa vikali na klabu kongwe za Simba na Yanga katika usajili wa dirisha dogo, lakini mambo yanavyokwenda inaonekana Simba wanaelekea kuwazidi ujanja Yanga kwa kuwa ndio waliozungumza nao kwa mara ya mwisho.

 

Kumbuka kuwa dirisha dogo linanukia, limepangwa kufunguliwa katikati ya mwezi ujao. Awali, Yanga ndiyo ilikuwa ya kwanza kuwania saini ya beki huyo kwenye usajili mkubwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu kabla ya dirisha dogo kumfuata huku Simba ikitajwa kuingia kwenye vita ya kuitaka saini ya beki huyo.

 

Hiyo ni baada ya beki huyo kuonyesha kiwango kikubwa katika mchezo wa kwanza wa kuwania kufuzu Afcon walipocheza na Equatorial Guinea wakifanikiwa kuwafunga mabao 2-1 mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku Mwamnyeto akicheza kati pamoja na Kelvin Yondani.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, Simba inawania saini ya beki huyo kwa ajili ya kuiboresha safu yao ya ulinzi ambayo inamtegemea Erasto Nyoni na Muivory Coast, Pascal Wawa pekee.

 

Mtoa taarifa huyo alisema wanataka kumsajili beki huyo baada ya Mbrazili, Tairone Do Santos kuonekana Kocha Mkuu wa timu hiyo kutoridhishwa na kiwango chake ambacho amekionyesha kwenye baadhi ya mechi ambazo amemuanzisha katika kikosi cha kwanza kwenye ligi.

 

Aliongeza kuwa mabosi baadhi wa timu hiyo tayari wamelipitisha jina la Mwamnyeto, hivyo wanasubiria Stars itakaporejea, haraka watakutana naye licha ya kuwepo mazungumzo ya awali wakati akiwa kwenye kambi ya timu hiyo iliyokuwa inajiandaa na mchezo na Guinea.

 

 

“Kama hivi sasa unavyoona Nyoni amejitonesha majeraha ya goti akiwa anaitumikia Stars, benchi la ufundi litapata shida katika kupanga kikosi chake kutokana na tatizo la majeraha aliyoyapata ambalo bado halijajua atakaa nje kwa muda gani.

 

“Hivyo, hatutaki hilo litokee katika timu, kikubwa tunataka kama ikitokea beki mmoja kati ya Wawa au Nyoni mmoja anaumia, basi benchi la ufundi haliumizi kichwa, haraka anapangwa mwingine mwenye uwezo kama wake, hivyo ni lazima uongozi usajili beki mwingine wa kati na anayepewa nafasi ni Mwamnyeto hadi hivi sasa.

 

“Lipo wazi kabisa Mwamnyeto ni beki mwenye uwezo wa kucheza nafasi hiyo na viongozi wameipenda hali yake ya kujiamini ya kucheza michuano mikubwa ya kimataifa, tayari mmoja wa viongozi alizungumza naye akiwa kambi ya Stars, tunasubiria Stars itakaporejea tukutane naye haraka,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Akimzungumzia beki huyo, Yondani alisema ni vizuri Yanga ikamsajili kwani ana ubora wa kutosha.

“Huyu ni kati ya mabeki bora wakongwe ambao wanang’aa hivi sasa, nimecheza naye na ninaona tunaweza kufanya vizuri pamoja. Yanga wasimuache aende Simba,” alisema Yondani.

 

Alipotafutwa Katibu wa timu hiyo, Dk Arnold Kashembe kuzungumzia hilo, alisema: “Bado hadi bodi ya timu itakapokutana na mara itakapokutana kupitia ripoti ya usajili ya kocha wetu Aussems, basi tutatoa taarifa lakini kwa haraka tayari zipo baadhi ya nafasi lazima ziongezwe wachezaji.”

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

 

Comments are closed.