Simba Yaipa Yanga Siku Tano Tu Kuandaa Silaha za Kuwaangamiza Ligi Kuu

Mwenyekiti wa Klabu, Murtaza Mangungu.

UONGOZI wa Simba SC, umesema hivi sasa nguvu zao wamezielekeza katika mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates, na siyo kwa Yanga SC.

 

Simba hivi sasa wapo kambini wakijiandaa kupambana na Orlando, mchezo wa kwanza utachezwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, kisha marudiano Aprili 24, Afrika Kusini.

 

Mara baada ya kumalizana na Orlando, Aprili 30, watacheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Mkapa, ambapo Simba wamesema watatumia siku tano tu kuandaa silaha za kuwaangamiza.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema wanafahamu Yanga, wanawafikiria, lakini wao hawawafikirii kabisa.

 

Ally alisema wanafahamu ukubwa wa mchezo dhidi ya Yanga, lakini kwa sasa nguvu zao wamezielekeza dhidi ya Orlando kuhakikisha wanapata ushindi nyumbani kabla ya kwenda kumaliza kazi Afrika Kusini.

 

“Tunafahamu watani wetu Yanga wanatuwaza sisi, lakini sisi tunawaza Orlando Pirates, kila mtu anawaza kwa ukubwa wake.

 

“Kabla ya mchezo dhidi ya Yanga, tutacheza dhidi ya Pirates mchezo ambao ni muhimu kwetu kama tukifanikiwa kupata ushindi nyumbani kabla ya kwenda kurudiana ugenini.

 

“Hivyo maandalizi yetu tumeyaweka dhidi ya Pirates, mara baada ya mchezo huo, tutakuwa na siku tano kujiandaa kucheza dhidi ya Yanga, hivyo tutatumia siku hizo kupanga mikakati ya kuwamaliza,” alisema Ally.

 

Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Yanga inaongoza ikiwa na alama 51, inafuatiwa na Simba yenye 41, zote zikicheza mechi 19, huku mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, ulishuhudiwa ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Simba 0-0 Yanga.

WILBERT MOLANDI NA LUNYAMADZO MLYUKA2179
SWALI LA LEO

Kupanda Kwa Bei ya Mafuta Nchini, Nini Kifanyike Kupunguza Bei?
Toa comment