The House of Favourite Newspapers

Simba Yakamilisha Hesabu Misri Kibabe, Yaongoza Kundi

0

SIMBA SC imekamilisha michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi kibabe hiyo ni baada ya kupunguza idadi ya mabao waliyofungwa mara ya mwisho ugenini kule Misri dhidi ya Al Ahly ya 5-0 na jana kumalizika kwa kufungwa bao 1-0.

 

Mustapha Ghorbal, raia wa Algeria ambaye alikuwa mwamuzi wa kati alionekana akilalamikiwa muda mrefu na wachezaji wa Simba kutokana na kupeta pale walipofanyiwa madhambi.

 

Mwamuzi huyo aliwaonyesha jumla ya kadi tatu za njano wachezaji wa Simba ambao ni Shomary Kapombe, Joash Onyango na Erasto Nyoni huku Al Ahly wakionyeshwa mara moja kwa kipa wake, El-Shenawy.

 

Bao pekee la ushindi kwa Al Ahly lilipachikwa na Mohamed Sherrif dakika ya 31 baada ya kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula kutema mpira aliokuwa ameokoa na kumkuta mfungaji aliyeusukuma nyavuni.

Huu ni mchezo wa kwanza kwa Simba inayonolewa na Kocha Mfaransa, Didier Gomes kupoteza katika hatua ya makundi msimu huu, baada ya mchezo wa jana sasa Simba inakuwa imeshinda mechi nne, sare moja na kupoteza mmoja hivyo imebaki kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 13 hivyo ilishakata tiketi ya robo fainali mapema tu.

 

Kwa upande wao Al Ahly, nao wametinga robo fainali baada ya kumaliza nafasi ya pili wakiwa na alama 11 walizopata kupitia michezo sita ambapo wameshinda mitatu, sare mbili na kupoteza mmoja.

Kiungo Luis ambaye aliwafunga Al Ahly katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa jijini Dar jana alikuwa kwenye uangalizi mkubwa chini ya mabeki wa Al Ahly ambao walimbana kila kona na kumfanya ashindwe kuonyesha makeke yake.

Katika mchezo mwingine wa kundi A ambao ulipigwa jana, AS Vita walipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Al Merreikh na hivyo kumaliza nafasi ya tatu na pointi zao saba huku Merreikh wakiwa mkiani na alama zao mbili.Kikosi cha Simba kilichoanza jana; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Hussein Tshabalala, Joash Onyango, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Clatous Chama, Jonas Mkude, Meddie Kagere, Lary Bwalya na Luis Miquissone.

 

Leave A Reply