Simba Yakataa Bilioni 3 Kumuuza Kagere

HUWEZI amini ila ndivyo mambo yalivyo, unaambiwa uongozi wa Simba umekataa kitita cha dola 1,500,000 (ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 3.5) ambacho kimetolewa na baadhi ya timu zinazomwania mshambuliaji wao raia wa Rwanda, Meddie Kagere.

 

Katika siku za hivi karibuni, Kagere amekuwa akiwindwa na timu mbalimbali za Afrika lakini pia nje ya Afrika kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuzifumania nyavu ambao amekuwa akiuonyesha uwanjani tangu ajiunge na Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya.

 

Baadhi ya timu hizo ni pamoja na TP Mazembe ya DR Congo, Raja Casablanca ya Morocco, Al Hilal ya Sudan pamoja na Zamalek ya Misri.

 

Timu hizo kwa pamoja zinadaiwa kumuhitaji Kagere na kila moja imetengea mamilioni ya fedha ili iweze kuinasa saini yake, lakini uongozi wa Simba chini ya mwekezaji mkuu wa timu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’ umegoma kumuachia.

 

Meneja wa Kagere, Mnyarwanda’ Patrick Gakumba, ameliambia Championi Jumatatu kuwa sababu kubwa ya viongozi wa Simba kukataa kumuuza Kagere ni kwamba bado wanahitaji huduma yake katika Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

“TP Mazembe wao walikuwa tayari kutoa dola 300,000 (zaidi ya Sh milioni 700), lakini pia Raja Casablanca ya Morocco pia inamhitaji Kagere na imeweka mezani kitita cha dola 400,000 (zaidi ya Sh milioni 936).

 

“Ukiachana na timu hizo, pia Zamalek pamoja na Al Hilal kila mmoja imetenga kitita cha dola 400,000 ili iweze kumsajili mchezaji huyo,” alisema Gakumba.

 

Kiasi chote hicho kilichowekwa na timu hizo nne zikiwemo za Waarabu, jumla yake ni dola 1,500,000 ambazo ni zaidi ya bilioni 3.5.

 

Kutokana na hali hiyo unaweza kusema kuwa Simba imekataa mabilioni ya fedha kwa kugoma kumuuza Kagere kwa madai kuwa bado inamhitaji.

 

Hivi karibuni tu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori aliliambia gazeti hili kuwa hawapo tayari kumuuza Kagere kwani wanamhitaji katika mbio zao kutetea ubingwa wao wa ligi kuu lakini pia mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo timu hiyo inashiriki hivi sasa. Simba wapo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa na pointi sita huku Kagere akiwa ndiyo kinara wa kufunga mabao katika timu hiyo akiwa nayo sita.

 

 

Hata hivyo, Gakumba amesema kuwa hana cha kufanya kwa sasa juu ya mchezaji wake huyo kwani anaheshimu mkataba alionao na Simba ila utakapomalizika ataamua cha kufanya.

 

 

“Kwa sasa namuombea tu kwa Mungu aendelee kuwa katika kiwango kizuri lakini pia aendelee kufunga ili thamani yake izidi kupanda zaidi na zaidi kwani wakati anatoka Gor Mahia fedha ambayo Simba waliitoa ilikuwa haizidi dola 100,000 (zaidi ya Sh milioni 230) lakini hivi sasa thamani yake imepanda zaidi,” alisema Gakumba.

 

Mkataba wa Kagere ndani ya Simba umebakia msimu mmoja na miezi miwili baada ya kusaini miaka miwili wakati anatua klabuni hapo akitokea Gor Mahia ya Kenya.

 

Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam

Toa comment