The House of Favourite Newspapers

Simba Yakataa Mabadiliko ya Ratiba ya Mchezo Dhidi ya Yanga

Dar es Salaam, Juni 12, 2025 – Klabu ya Simba SC imethibitisha kuwa itaingia uwanjani kushiriki mchezo namba 184 dhidi ya Yanga utakaochezwa tarehe 15 Juni 2025, kama ulivyopangwa rasmi na Bodi ya Ligi Kuu.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa na klabu hiyo, Simba imesisitiza kuwa haitambui mabadiliko yoyote yatakayojaribu kuahirisha au kubadilisha tarehe ya mchezo huo, ikieleza kuwa hatua hizo ni batili na kinyume na taratibu za uendeshaji wa mpira wa miguu nchini.

“Simba SC haitashiriki mchezo wowote wa namba 184 isipokuwa ule uliopangwa kuchezwa Jumapili, Juni 15, 2025,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa, unatajwa kuwa ni miongoni mwa mechi za kusisimua zaidi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ukikutanisha wapinzani wa jadi katika kile kinachojulikana kama “Kariakoo Derby.”

Kauli ya Simba imekuja katikati ya tetesi kuhusu uwezekano wa kubadilishwa kwa ratiba ya mechi hiyo, huku mashabiki na wadau wa soka wakisubiri tamko rasmi kutoka kwa Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).