The House of Favourite Newspapers

Simba Yamuacha kocha Dar

0

MAPEMA wiki ijayo, kikosi cha Simba kinatarajiwa kuanza safari kuelekea Botswana kucheza mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy. Mchezo huo umepangwa kuchezwa Oktoba 17, kisha marudiano ni Oktoba 22 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

 

Taarifa ambazo Spoti Xtra limezipata, zinasema kwamba, Simba itaenda nchini humo bila ya kocha wake msaidizi, Seleman Matola ambaye anajiandaa kwenda Morogoro kuendelea na kozi ya ukocha ya Shirikisho la Soka Afrika CAF diploma B ambayo akimaliza itamuwezesha kukaa kwenye benchi kama kocha msaidizi kwenye mechi za CAF.

 

Matola alianza kusoma kozi hiyo takribani miezi mitatu iliyopita ambapo hapa kati ilisimama baada ya kumaliza awamu ya kwanza na sasa analazimika kwenda kumalizia masomo yake.

 

“Matola hataenda Botswana wakati timu ikienda kucheza dhidi ya Jwaneng Galaxy kwa sababu hivi karibuni ataenda Morogoro kumalizia masomo yake,” kilisema chanzo.

 

Wakati Matola akishindwa kusafiri na timu, Kocha Hitimana Thiery, anatarajiwa kuanza kazi rasmi ya kuinoa timu hiyo ambapo awali suala la vibali vyake vya kazi vilikuwa vinamzuia.

 

Hitimana ambaye Septemba 10, mwaka huu alitambulishwa kuwa kocha msaidizi wa Simba, ameongezwa kwenye benchi la ufundi la timu hiyo kutokana na kukidhi vigezo ambavyo CAF wanavihitaji.

 

Kuongezwa kwa Hitimana, kumekuja baada ya Kocha Didier Gomes kuonekana hana sifa za kuiongoza Simba kama kocha mkuu katika michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) msimu huu kwa kuwa ana leseni ya UEFA A.

 

Kwa mujibu wa Kanuni za CAF, makocha wakuu wanapaswa kuwa na leseni ya CAF A kwa wale waliosomea ndani ya Afrika pamoja na UEFA pro license kwa wale waliochukua mafunzo ya ukocha barani Ulaya.

 

“Suala la Kocha Hitimana kupata vibali, lipo kwenye hatua za mwisho kabisa na kabla ya timu haijaenda Botswana, kila kitu kitakuwa sawa na rasmi ataanza kazi ya kuifundisha timu yetu kwenye mechi mbalimbali.

 

“Kama mnavyofahamu kwamba kocha wetu mkuu Gomes ana changamoto ya leseni yake kwa mujibu wa kanuni za CAF, hivyo uwepo wa Hitimana tunaamini hakitaharibika kitu,” kilisema chanzo hicho.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Hitimana alisema: “Mpaka kufikia mchezo dhidi ya Jwaneng mambo yatakuwa yameshakamilika na tayari nitakuwa nimepata kibali cha kufanya kazi.”

Leave A Reply