Kiungo wa Yanga, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.
Said Ally na Omary Mdose
KIUNGO wa Yanga, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, atakaa nje ya uwanja kwa siku zisizofahamika kutokana na kupata majeraha ya enka wakati akiitumikia timu yake ilipocheza dhidi ya Simba, wikiendi iliyopita.
Katika mchezo wa wikiendi ambao Yanga ilishinda kwa mabao 2-0, Niyonzima alicheza kwa dakika 53 kabla ya kumpisha Simon Msuva baada ya kuumia kutokana na kugongwa na beki wa Simba, Hassan Kessy. Kutokana na kupata majeraha hayo, Niyonzima alilazimika kukosa mazoezi ya jana asubuhi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Karume, Dar, wakati timu yake ilipokuwa ikijiandaa na mchezo wa leo wa Kombe la FA dhidi ya JKT Mlale utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Kabla ya kuanza kwa mazoezi hayo, Championi lilimshuhudia Niyonzima akiwa na makocha wake, Hans van Der Pluijm (kocha mkuu) na Juma Mwambusi (msaidizi) wakiongea huku akilalamikiwa iweje mara kwa mara awe anaumwa yeye tu, hali ambayo wanahisi ni uongo lakini mwenyewe anadai ni mgonjwa kweli.
Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, ameliambia Championi Jumatano kuwa, Niyonzima aliumia katika mchezo dhidi ya Simba na jana Jumanne walitarajia kumpeleka hospitali ili kumfanyia uchunguzi zaidi wa tatizo lake.
“Niyonzima leo (jana) ameshindwa kufanya mazoezi kutokana na kupata majeraha tulipocheza dhidi ya Simba, bado hatujajua zaidi ukubwa wa tatizo lake na leo (jana) tunatarajia kumpeleka hospitali kufanyiwa uchunguzi,” alisema Saleh.
Katika hatua nyingine, Saleh aliongeza kuwa, wapinzani wao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Cercle de Joachim kutoka Mauritius, wanatarajia kuingia nchini kesho Alhamisi kwa ajili ya mechi ya marudiano inayotarajiwa kupigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa, baada ya mchezo wa awali Yanga kushinda 1-0.