Kartra

Simba Yanasa Siri za Kaizer

JANA Jumatano, Kaizer Chiefs ilitarajiwa kucheza mechi ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini dhidi ya Moroka Swallows, ambapo Simba walipanga kuufuatilia mchezo huo kwa lengo la kuzinasa mbinu za wapinzani wao hao.

 

Uamuzi wa Simba kufanya hivyo umekuja ikiwa ni kuelekea mchezo wao wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Jumamosi hii.

 

Kaizer Chiefs na Simba, zinatarajiwa kupambana kwenye Uwanja wa FNB uliopo Johannesburg, Afrika Kusini, kisha marudiano ni Mei 22, mwaka huu Uwanja wa Mkapa, Dar.

 

Kwa sasa Simba tayari ipo nchini Afrika Kusini ikiendelea na maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo huo wa Jumamosi.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, alisema kuwa wanawatazama wapinzani wao kwa ukaribu ili kujua namna ya kuwakabili kwa kuwa wanahitaji matokeo mazuri.

 

“Kiukweli bado tunaendelea kuwafuatilia wapinzani wetu kwani ni timu nzuri na ina wachezaji ambao wanaleta ushindani, kabla ya hapo tuliangalia mechi zao zilizopita na bado tunawafuatilia ili kujua namna gani wanafanya ndani ya uwanja.

“Kuna mechi ambayo wanacheza hivi karibuni (jana Jumatano), pia tunawafuatilia kisha tutajua namna gani tunaweza kupata ushindi dhidi yao. Kikubwa ni kwamba Watanzania waendelee kutuombea kwani ushindani ni mkubwa,” alisema Matola.

 

TIZI LAO

Simba baada ya kufika Afrika Kusini mchana wa juzi Jumanne, usiku walifanya mazoezi kwenye Viwanja vya Discovery Soccer Park – Sandton.Taarifa kutoka kambini huko Afrika Kusini, zinasema kwamba, katika mazoezi hayo ya awali, Kocha Gomes alianza taratibu ili kurudisha hali ya utimamu na kuondoa uchovu wa safari kwa wachezaji, kabla ya jana kufanya mazoezi ya mbinu kwa nguvu.

 

MORRISON ATUA SAUZ

Katika msafara wa wachezaji 24 ulioondoka juzi Jumanne, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Bernard Morrison hakuwepo huku ikielezwa kwamba kuna mambo anashughulikia na ataungana na wenzake jana.Mapema jana, Morrison alianza safari ya kuelekea Afrika Kusini kuungana na wenzake kuongeza nguvu jambo ambalo Wanasimba wameshusha pumzi baada ya awali kusemekana nyota huyo hasafiri.

 

REKODI ZA KAIZER CHIEFS NYUMBANI

Kuelekea mchezo huo, rekodi zinaonesha kwamba, Kaizer Chiefs pindi wanapocheza na vigogo nyumbani kwao katika mashindano mbalimbali, wameonekana kuwa tishio.Kwenye Uwanja wa FNB, Kaizer Chiefs haijapoteza mchezo wowote katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu licha ya kucheza dhidi ya timu ngumu ikiwemo Wydad Casblanca, Petro de Luanda na Horoya AC.

 

Kuelekea mcheo huo dhidi ya Simba, Mkurugenzi wa Masoko wa Kaizer Chiefs, Jesica Moutang, alisema: “Tunatakiwa kufikia malengo yetu ambayo ni kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, hatutaki kuipoteza hii nafasi tuliyoipata.“Malengo yetu ni kutawala soka la Afrika miaka ijayo, tunaanza sasa kwa ajili ya mipango ya baadaye, tupo tayari kwa ajili ya kupambana ili tusonge mbele.”

STORI: LUNYAMADZO MLYUKA NA MARCO MZUMBE


Toa comment