Simba, Yanga Acheni Kulia Njaa, Amkeni Sasa
MAKALA: MUSA MATEJA – SAUZI | CHAMPIONI JUMATANO |HABARI
KLABU kongwe nchini Tanzania za Simba na Yanga, zimekuwa zikilia njaa kila mwaka huku zikishindwa kujiendesha zenyewe zikitegemea pesa za matajiri wao mmoja mmoja kitu ambacho ni hatari ikitokea siku matajiri wao wamepata matatizo.
Yanga iliyoanzishwa mwaka 1935 huku Simba ikifuatia mwaka mmoja mbele, mpaka leo hii zimeshindwa kutumia fursa ya ukongwe wao katika kujitengenezea pesa, badala yake zinaishi kwa staili ya ombaomba.
Hivi karibuni, klabu hizo zilimaliza mkataba na Kampuni ya Bia ya Kilimanjaro ambayo ilikuwa ikizisaidia vifaa pamoja na usafiri, baada ya hapo zimekosa wadhamini hali iliyosababisha kwa kipindi kifupi kuanza kulia njaa.
Yanga kwa sasa hakuna hali nzuri kifedha na hiyo ni baada ya mwenyekiti wake, Yusuf Manji kukumbwa na matatizo, wachezaji na watendaji wengine klabuni hapo, wakaanza kuishi kwa kuungaunga. Kuna baadhi ya wachezaji waligoma kushinikiza kulipwa malimbikizo yao ya madeni.
Huku Simba na Yanga zikilia njaa na kushindwa kutumia fursa zilizo nazo, nyuma yao kwa muda mrefu Watanzania wengine wamekuwa wakipiga pesa ndefu kupitia majina ya klabu hizo mbili.
Watanzania wamekuwa wakiuza jezi, kofia, skafu na hata masweta yenye nembo ya klabu hizo, lakini pesa hizo haziingii mifukoni mwa Yanga wala Simba, zinabaki kwa Watanzania hao wajanja.
Hali hiyo ni tofauti na hapa Afrika Kusini ambapo tangu nimewasili wiki iliyopita, nimegundua klabu za huku zinatumia vema majina na nembo zao kujipatia pesa.
Katika uchunguzi wa muda mfupi, nimeweza kulibaini hilo kwa klabu tatu maarufu nchini hapa ambazo ni Orlando Pirates, Kaizer Chiefs na Mamelodi Sundowns.
Orlando Pirates:
Klabu ya Orlando Pirates inayodhaminiwa na Kampuni ya Adidas, inauza jezi zake za msimu huu kwa randi 699 ambayo ni sawa na Sh 118,830 za Kitanzania, lakini mbali na kuuza jezi zao, kuna bidhaa nyingine orijino wanazouza kama ‘track suit’ kwa randi 999, sawa na Sh 169,830.
Kaizer ChiefS:
Klabu hii inadhaminiwa na Nike ambapo kupitia kampuni hiyo inajiingizia mamilioni ya pesa kila mwaka kwani inauza vitu vyake orijino tofauti na timu zetu za Tanzania.
Ukienda dukani wanapouza bidhaa zao, utakuta jezi inauzwa randi 699 ambayo ni sawa na Sh 118,830 za Kitanzania. Si hivyo tu, bali utakuta kofia zinazouzwa kwa randi 499 (sawa na Sh 82,918 za Kitanzania), lakini pia ‘track suit’ ni randi 999 (sawa na Sh 169,830).
Jezi ya kipa ni tofauti na ya wachezaji wengine ambapo jezi yake imepunguzwa bei, kwa sasa inauzwa randi 699 (sawa na Sh 118,830) kutoka randi 1,299 (sawa na Sh 220,830).
Mamelodi Sundowns:
Ukija katika Klabu ya Mamelodi Sundowns, maarufu kwa jina la utani la ‘The Brazilians’, hii inadhaminiwa na Kampuni ya Puma. Jezi zake ukienda dukani wala hazitofautiani bei na zile za Kaizer Chief na Orlando Pirates.
Katika ardhi ya Afrika Kusini, hakuna vitu feki kama Bongo, hivyo Mamelodi Sundowns wanauza jezi zao orijino kwa randi 699, ambayo ni sawa na Sh 118,830 za Kitanzania.
Ukikaa chini na kupiga hesabu bidhaa zinazouzwa na klabu hizo, utagundua kwamba kwa mwaka wana uwezo wa kuingiza kiasi kikubwa cha pesa, lakini Simba na Yanga kila mwaka huwa zinatangaza hasara zilizopata.
Cha kujiuliza ni kwamba kitu gani ambacho kinashindikana kwa timu zetu kongwe wakati ukiangalia zenyewe zina miaka mingi kuliko hizi za huku?
Ukipita Mitaa ya Kariakoo, Ilala au hata Manzese, utakuta jezi ya Simba au Yanga inauzwa kwa kiwango cha chini cha Sh 5,000 ambayo inaishia mikononi mwa wajanja tu, lakini katika maduka ya huku Afrika Kusini, jezi ya Orlando, Kaizer na Mamelodi ile ya bei ya chini inaweza kuwa mara 15 na nusu ya ile ya Manzese au Ilala, lakini kitu kizuri ni kwamba klabu za huku pesa hizo za mauzo ya jezi haziishii mikononi mwa wajanja, bali zinafika moja kwa moja kwa wahusika klabuni.