The House of Favourite Newspapers

Simba, Yanga Sawa Lakini Wapeni Heshima Waandishi

Wachezaji wa timu ya Simba.

 

MCHEZO wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Yanga uliochezwa wikien­di iliopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, ulimalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa ‘kiraka’ wake, Erasto Nyoni.

 

Mchezo huo ambao ulikuwa ni wa watani wa jadi, ulikuwa na up­inzani mkali kwa dakika zote tisini, lakini ni wazi Simba walionekana kuwa imara zaidi tofauti na Yanga kutokana na kufanya masham­bulizi mengi ambayo yalikuwa ni ya uhakika kwa muda wote.

 

Ushindi wa Simba dhidi ya Yan­ga sasa umewapa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kufikisha pointi 62. Wameiacha Yanga kwa pointi 14. Wapinzani hao kutoka Jangwani kwa sasa wanashika na­fasi ya tatu wakiwa na pointi 48, huku Azam FC ikiwa na pointi 49 kwenye nafasi ya pili.

Hongera Simba kwa ushindi dhi­di ya Yanga lakini pia kwa kuonye­sha soka la kiwango cha juu kwa timu zote mbili licha ya mapun­gufu machache yaliyotokea ndani ya uwanja ambayo naamini hay­awezi kupunguza ubora wa mch­ezo wenyewe.

 

Lakini nje ya mchezo huo kuna jambo moja kubwa lilitokea uwan­jani hapo hasa upande wa waandi­shi wa habari na waliopewa ju­kumu la kusimamia usalama hasa pale kwenye mlango mkuu wa kuingilia vyumbani, waliamua kuzuia kufuatia agizo lililotolewa na mmoja wa ‘makomandoo’ wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

 

Hilo limezoeleka na ndiyo ume­kuwa utaratibu katika mechi zote mara baada ya mchezo waandishi wa habari kuingia katika eneo hilo kwa kufanya mahojiano na mako­cha pamoja na wachezaji.

 

Ajabu, baada ya mchezo huo, wana usalama hao waliokuwa wamewekwa katika eneo hilo hawakutaka kabisa kuruhu­su waandishi kuingia licha ya kuwa na vitambulisho ambavyo vimetolewa na TFF na kufanya tushindwe kufanya kazi yetu kwa wakati lakini katika vurumai hizo zilisababisha baadhi ya waandishi na viongozi wa Yanga na Simba kupigwa virungu bila ya sababu za maana.

 

Watu wa usalama wanaopewa kazi ya kulinda viwanjani wame­kuwa wakifanya kazi vizuri wakiwa chini ya Mkuu wa Usalama wa TFF, Inspekta, Hashim Abdallah, lakini inapofikia hatua ya waandishi ku­zuiwa kutimiza wajibu wetu wa ki­taaluma, hilo linakuwa tatizo kwa sababu haipendezi kutunyanyasa kwa jambo ambalo lipo wazi.

 

Hii siyo mara ya kwanza kutokea kwa tukio la aina hii kwa upande wa waandishi kwa kuwa wapo baadhi ya wahusika wanakuwa hawana ufahamu na suala la vi­tambulisho vya TFF kwa watu am­bao wanakuwa navyo viwanjani.

 

Kama mtaendelea kuruhusu uhuni huu wa kutuzuia tusifanye kazi yetu kwa wakati mtakuwa hamtendi haki na mwisho wa siku ule ushirikiano wetu utageuka kuwa uadui. Muda wa kulifanyia kazi suala hilo bado upo.

 

Hivyo basi, huu ndiyo wakati wenu TFF inayoongozwa na Rais Wallace Karia, pamoja na mkuu wa usalama viwanjani, Inspekta Hashim Abdallah kuanza ku­lifanyia kazi jambo hilo ili wakati mwingine lisiweze kujirudia kwa kuwa tumekuwa tunashirikiana kwenye mambo mengi ya kikazi bila ya kuwa na matatizo.

NA IBRAHIM MUSSA | ACHA NISEME

 

Comments are closed.