The House of Favourite Newspapers

Simba: Yanga Wanakufa Nne – Video

0

RAHA ya mchezo wa Simba na Yanga hupatikana nje na ndani ya uwanja, huku nje ni tambo za mashabiki na wasemaji na ndani ya uwanja ni pale mmoja anapofungwa.

 

Haji Manara, Ofisa Habari wa Simba SC ameweka wazi kuwa miongoni mwa sifa zitakazoipa Simba ushindi kwenye dabi ya leo dhidi ya Yanga ni kwa sababu kocha wao, Didier Gomes Da Rosa anawajua sana wachezaji wa Yanga kuliko hata kocha wao anavyowafahamu wachezaji wa Simba.

 

Manara aliyasema hayo jana alipotinga studio za Global Radio na kufanya mahojiano kwa urefu kuelekea kwenye dabi hiyo.

 

Ofisa habari huyo alisema moja ya mbinu ambazo Gomes anatumia ili kupata ushindi ni yeye pamoja na benchi lake la ufundi ni kutenga muda kwa ajili ya kusoma wapinzani wao na hiyo ni sababu kubwa sana yake yeye kujua sana wachezaji wa Yanga.

 

“Gomes ni mtu wa mpira. Kama mwalimu, kila wakati anawasoma wapinzani wake kabla ya kukutana nao. Yeye ni bingwa wa kubadilisha mbinu kutokana na aina ya wapinzani wake na mchezo wenyewe.

 

“Nina uhakika kuwa Gomes anawajua wachezaji wa Yanga kuliko hata Nabi anavyowajua wachezaji wake, na hii ndiyo itakuwa sababu kubwa ya Simba SC kupata ushindi kesho,” alisema Manara.

 

YANGA ANAKUFA 4-0

Baada ya kutamba kuwa kocha Gomes ni fundi wa mbinu na anawajua vema Yanga, Manara alisema kama mchezo huo utakuwa hauna ujanjaujanja basi Yanga anakufa 4-0 huku akipigiwa mpira mwingi sana.

 

“Yanga anafungwa mabao 4-0, kama hakuna ujanja ujanja, wala zile sijui refa kapuliza filimbi bila sababu, wala kujifanya kubalansi muda, wanakufa nne, yaani hicho ni kiwango cha chini lakini vinginevyo watakufa nyingi zaidi.

 

MORRISON KUFANYA BALAA NZITO

“Morrison (Bernard) amelibeba balaa, dakika atakazokaa uwanjani ni hatari kwa sababu kwenye nchi hii hakuna mchezaji mwenye uchu kama Morrison. Yule ni mchezaji pekee ambaye akili yake huwa inawaza kwenda golini tu, sasa sijui kama ataanza au vipi lakini hata akipewa dakika 12 itakuwa ni balaa.

 

HANA PRESHA, ATOA ONYO KWA WAAMUZI

“Sina presha ya kucheza na Yanga, presha yangu huwa pale tunapocheza na timu kubwa kama Al Ahly au Kaizer Chiefs, lakini siyo Yanga kwa sababu mara zote wanashinda kwa ujanja.

 

“Hakuna mchezaji ambaye tunaweza kumuhofia ndani ya Yanga, ukubwa wa Yanga hauwezi kufikia Al Ahly, Al Merrikh na Vita ambao sisi tumeshacheza nao na tukapata matokeo wakiwa kwao, ije kuwa Yanga bwana!

 

“Tunawaheshimu tu, lakini hatuwezi kuwahofia, wachezaji wa kwenye mechi kama hii, siku moja kabla wanakuwa wanacheza Play Station Game tu kule kimbinu hawana presha.

 

“Na niseme kitu kimoja, refarii wa kesho (leo) hatutaki kupendelewa, tunataka refarii afuate haki zote (kanuni) 17 za soka. Ikitokea Yanga wametufunga 5-0 na mchezaji wao akafanyiwa faulo kwenye boksi, refa toa penalti na kama kuna kadi nyekundu apewe mchezaji wetu na Simba tufungwe bao sita.

 

“Lakini sisi tunachotaka ni haki itendeke, asipendelewe wala kudhurumiwa mtu, watu wanataka burudani maana hawa wenzetu tunajua watakuja kugongana kwahiyo refa awe makini.”

 

Ikumbukwe kwamba mzunguko wa kwanza ubao ulisoma Yanga 1-1 Simba ni Michael Sarpong wa Yanga na Joash Onyango wa Simba walicheka na nyavu.

ISSA LIPONDA NA MANJIRO LYIMO

 

Leave A Reply