The House of Favourite Newspapers

Simba Yatua Kwa Straika Wa Mabao DR Congo

0

IMEELEZWA kuwa, uongozi wa Simba upo katika mchakato wa kumsajili mshambuliaji wa kati kutoka DC Motema Pembe inayoshiriki Ligi Kuu ya DR Congo, Kadima Kabangu kwa ajili ya kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji la timu hiyo.

 

Simba ikiwa inahitaji huduma ya mshambuliaji huyo anayetajwa kuwa na njaa ya mabao, katika eneo la ushambuliaji wa kati tayari ina washambuliaji wanne ambao ni Meddie Kagere, John Bocco, Chriss Mugalu na Charles Ilanfya.

 

Wakala wa mchezaji huyo, Kazadi Kabue, ameliambia Spoti Xtra kwamba, uongozi wa Simba umemuulizia mteja wake kuhusiana na masuala ya usajili wakihitaji saini yake.

 

Alisema kuwa, mshambuliaji huyo bado ana mkataba na Motema Pembe, hivyo kama kweli Simba wapo siriazi na mteja wake wanatakiwa kuvunja mkataba huo.“

 

Ni kweli Kadima Kabangu ameuliziwa na viongozi wa Simba, wameonesha kuwa wanahitaji kumsajili mteja wangu, mimi sina cha kuongea kingine zaidi ya kuhitaji kusubiri wakati wa usajili ukifika tuone inakuwaje.

 

“Lakini wanachotakiwa kufahamu ni mteja wangu huyu ana mkataba na timu yake ya sasa ya Motema Pembe, hivyo wanatakiwa kuvunja huo mkataba kama kweli wana nia naye, ngoja tusubiri tuone kitatokea nini,” alisema wakala huyo.Kabangu aliyezaliwa Kinshasa, DR Congo Juni 15, 1993, kwa sasa ana miaka 27, tayari ameitumikia timu ya taifa ya DR Congo.

 

Kwa upande wa klabu, amezichezea FC Lupopo ya DR Congo, Budapest Honvéd (Hungary), Shirak (Armenia), Maghreb de Fès (Morocco) na kwa sasa ni mali ya DC Motema Pembe.

 

Simba kwa sasa inasaka mshambuliaji mwingine wa kati baada ya Mugalu kuwa na majeraha ya mara kwa mara, huku Ilanfya akikosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza ambapo hivi karibuni, Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Mwina Kaduguda, alisema lazima eneo hilo waliboreshe katika usajili huu wa dirisha dogo unaotarajiwa kufunguliwa Desemba 15, mwaka huu.

STORI NA MARCO MZUMBE, Dar es Salaam

Leave A Reply