The House of Favourite Newspapers

Simba yawatengea Waarabu dakika 180

Kikosi cha timu ya Simba.

UONGOZI wa Simba umepanga mipango kabambe ya kuitumia michezo yao ya karibuni dhidi ya Azam FC na Lipuli FC yeye dakika 180 kama sehemu ya maandalizi yao kabla ya kuvaana na Waarabu JS Saoura kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Simba ndani ya wiki chache zijazo watakuwa na michezo ya ligi ambapo walianza jana Jumanne kwa kucheza na African Lyon kisha Ijumaa hii watacheza na Azam kisha wataenda kucheza na Lipuli mkoani Iringa.

 

Simba watasafiri kwenda Algeria kwa ajili ya kucheza mechi ya marudiano na wenyeji wao JS Saoura katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ile ya kwanza Simba kushinda mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar. Mechi hii itapigwa Machi 9.

 

Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori ameliambia Championi Jumatano, kuwa mechi hizo za ligi ambazo watacheza katika siku za karibuni zitakuwa msaada tosha kwao kwa ajili ya mechi yao hiyo ya kimataifa.

 

“Tuna ratiba ngumu ya mechi za karibukaribu katika Ligi Kuu Bara ambazo kwetu tunatakiwa kupata ushindi kwa ajili ya kujiweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi.

 

“Lakini nje ya kupata pointi kwenye mechi hizo zote, mechi hizo tunazichukulia kama sehemu yetu ya maandalizi kwa ajili ya mechi yetu ya kimataifa dhidi ya JS Saoura.

 

“Unajua hakuna muda wa kujiandaa kwa ajili ya mechi hiyo zaidi ya kucheza mechi hizo, kwa hiyo tutakachokifanya ni kupata pointi tatu katika kila mechi lakini mawazo yetu pia tunaichukulia michezo miwili yenye dakika 180 kama sehemu ya maandalizi yetu kwenye mechi yetu ya kimataifa,” alisema Magori.

Comments are closed.